Abu Sa’iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

”Ee Allaah! Nipe uhai nikiwa masikini na unifishe masikini na unikusanye katika mkusanyiko wa masikini.”[1]

Ameipokea Ibn Maajah.

Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia mfano wake kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na akaongeza:

‘Aaishah akasema: “Kwa nini, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Kwa sababu wataingia Peponi miaka arubaini kabla ya matajiri wao. Ee ´Aaishah! Usimrudishe nyuma masikini, hata ikiwa ni kwa nusu ya tende. Ee ´Aaishah! Wapende masikini na kuwa karibu nao, ili Allaah akufanye kuwa karibu siku ya Qiyaamah.”[2]

Abu Dharr amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ameniusia kuwapenda masikini na kuwasogelea karibu.”[3]

Ameipokea Ahmad na wengineo.

Mu’aadh (Radhiya Allaahu ‘anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Nakuomba kuweza kufanya matendo mema, kuacha maovu na kuwapenda maskini.”[4]

Maskini waliokusudiwa katika Hadiyth hizi na zinazofanana na hizi ni wale ambao nyoyo na miili yao ni duni, yenye kumnyenyekea na kumuogopa Allaah. Mara nyingi sifa hiyo inapatikana kwa kutokuwa na mali, kwa sababu hupelekea kupata kiburi. Hadiyth ya Anas (Radhiya Allâhu ´anh) inathibitisha hilo, licha ya kwamba mlolongo wa wapokezi wake ni dhaifu. Abu Dharr (Radhiya Allaahu ‘anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Ufukara ni ufukara wa nafsi na utajiri ni utajiri wa moyo.”[5]

Ameipokea na an-Nasaa’iy.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Utajiri ni utajiri wa nafsi.”[6]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Kwa ajili hiyo Imaam Ahmad, Ibn ´Uyaynah, Ibn Wahb na maimamu wengine walisema kwamba umasikini ambao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alijilinda nao ni umasikini wa nafsi. Yule ambaye moyo wake unanyenyekea na kumcha Allaah (‘Azza wa Jall) ni maskini ingawa atakuwa tajiri kifedha. Kwa sababu unyenyekevu wa moyo hauachi unyenyekevu wa viungo vya mwili. Ikiwa mwili wa mtu unaonyesha kuogopa na kunyenyekea na sambamba na hilo moyo wake hauogopi wala haunyenyekei, basi uhakika wa mambo ni kwamba ni mwenye kiburi. an-Nasaa’iy na wengineo wamepokea:

“Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipita kwenye barabara ambayo alikuwepo mwanamke mweusi. Bwana mmoja akasema: “Njia iko wapi?” Akasema: ”Akitaka atashika njia ya kulia na akitaka atashika njia ya kushoto.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema: “Mwacheni, kwani ni mwenye jeuri.” Wakasema: “Mtume wa Allaah! Anamaanisha kuwa yeye ni masikini.” Ndipo akasema: “Ni kitu kiko moyoni mwake.”[7]

[1] at-Tirmidhiy (2352). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy” (2352).

[2] at-Tirmidhiy (2352). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy” (2352).

[3] Ahmad (5/159 na 173) na Ibn Hibbaan (449), ambaye ameisahihisha.

[4] at-Tirmidhiy (3233). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy” (3233).

[5] an-Nasaa’iy (9/157) na al-Haakim (4/327), ambaye ameisahihisha.

[6] al-Bukhaariy (6447) na Muslim (1741).

[7] an-Nasaa’iy (6/143).

  • Muhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn ´Abdur-Rahmaan bin Rajab al-Hanbaliy (afk. 795)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Khushuu´ fiys-Swalaah, uk. 89-94
  • Imechapishwa: 24/11/2025