al-Hasan (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kuna watu ambao wameweka unyenyekevu katika nguo zao na kiburi kwenye mioyo yao; wanavaa mavazi ya nje. Naapa kwa Allaah! Wana kiburi zaidi kwa nguo zao kuliko mwenye kiti cha enzi kwa kiti chake na mwenye nguo ya hariri kwa hariri yake.”

Imesihi kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikanusha uvaaji wa nguo nzuri na viatu vizuri kuwa ni sehemu katika kiburi na akasema:

“Kiburi ni kuikataa haki na kuwadharau watu.”[1]

Hii ni dalili ya wazi kabisa kwamba mavazi mazuri sio katika kiburi. Hapana vyenginevyo kiburi kinakuwa ndani ya moyo kwa namna ya kwamba mtu akaacha kuinyenyekea haki kwa sababu ya kuifanyia kiburi. Kuwadharau watu ni kule kuwashusha na kuwapunguza. Kwa hivyo yule ambaye anaikweza nafsi yake kwa njia ya kwamba anawadharau watu kwa kujiona kuwa ni mkubwa na anakataa kuinyenyekea haki basi ni mwenye kiburi hata kama nguo na viatu vyake sio vizuri.

Yule mwenye kujiepusha kuvaa nguo nzuri kwa ajili ya kumnyenyekea Allaah na kuogopa asiingizwe na kitu katika kiburi basi amefanya vyema. Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ‘anhumaa) alikuwa akifanya hivyo. Isitoshe hayo yanafahamishwa na Hadiyth isemayo:

“Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliswali kwenye Khamiyswah iliyo na mifumo na akatazama mifumo yake. Alipomaliza akasema: “Ipelekeni kanzu hii kwa Abu Jahm na mniletee Anbajaaniyah ya Abu Jahm. Inanishughulisha kutokamana na swalah yangu.”[2]

[1] Muslim (91).

[2] Muslim (556).

  • Muhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn ´Abdur-Rahmaan bin Rajab al-Hanbaliy (afk. 795)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Khushuu´ fiys-Swalaah, uk. 95-97
  • Imechapishwa: 24/11/2025