24. Idadi ya wakazi wa Peponi na idadi ya wakazi wa Motoni imekwishapangwa

Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

46 – Allaah amekwishajua tokea mwanzo idadi ya ambao wataingia Peponi na idadi ya watakaoingia Motoni. Idadi hiyo haitozidi na wala haitopungua. Aliyajua pia matendo yao watakayofanya.

MAELEZO

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) anaashiria Hadiyth iliyosimuliwa na ´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye amesema:

”Mtume wa Allaah alitujia na kwenye mikono yake akiwa na vitabu viwili; kitabu kimoja kwenye mkono wa kulia na kitabu kingine kwenye mkono wa kushoto. Akasema: ”Mnajua ni nini vitabu viwili hivi?” Tukasema: ”Hapana, ee Mtume wa Allaah, isipokuwa ukitueleza.” Akasema kuhusu kile kitabu kilicho kwenye mkono wa kulia: ”Hiki ni Kitabu cha Mola wa walimwengu. Ndani yake mna majina ya wakazi wa Peponi na majina ya baba zao na makabila yao. Baada ya yule mtu wa mwisho kupigwa muhuri hakutozidishwa wala kupunguzwa ndani yake.” Kisha akasema kuhusu kile kitabu kilicho mkononi mwake mwa kushoto: ”Hiki ni Kitabu cha Mola wa walimwengu. Ndani yake mna majina ya wakazi wa Motoni na majina ya baba zao na makabila yao. Baada ya yule mtu wa mwisho kupigwa muhuri hakutozidishwa wala kupunguzwa ndani yake.” Wakasema Maswahabah zake: ”Ee Mtume wa Allaah! Kuna maana gani ya kutenda ikiwa mambo yamekwishapangwa?” Akajibu: ”Jipindeni kwelikweli na fanyeni kati na kati. Hakika mtu atakayeingia Peponi atamaliza kwa kufanya matendo ya watu wa Peponi, pasi na kujali matendo atayotangulia kufanya. Mtu atakayeingia Motoni atamaliza kwa kufanya matendo ya watu wa Motoni, pasi na kujali matendo atayotangulia kufanya.” Kisha akaonyesha kwa mikono yake kama vile anawatupa kisha akasema: ”Mola wenu amemaliza na waja:

 فَرِيقٌ فِي الْجَنَّةِ وَفَرِيقٌ فِي السَّعِيرِ

”Kundi litakuwa katika Pepo na kundi katika moto uliowashwa vikali mno.”[1][2]

Ameipokea at-Tirmidhiy, na yeye na wengine wameisahihisha. Nimeitaja katika ”Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah”[3].

[1] 42:07

[2] at-Tirmidhiy (2141) na Ahmad (6563). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy” (2141).

[3] Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah (848).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah – Sharh wa Ta´liyq, uk. 39-40
  • Imechapishwa: 23/09/2024