237. ´Aqiydah ya kati na kati baina ya Jabriyyah na Qadariyyah

´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah iko kati na kati baina ya Jabriyyah na Qadariyyah. Jabriyyah wamechupa mipaka katika kuthibitisha makadirio mpaka wakafikia kumkanushia mja kuwa na khiyari ya kuchagua. Wanaona kuwa mja hana uwezo wa kujichagulia na kwamba matendo yake yote ametenzwa nguvu juu yake. Kwa maana nyingine ni kama mashine inayoendeshwa na makadirio. Hana khiyari ya kujichagulia swalah, swawm na matendo yake mengine. ´Aqiydah hii ni batili.

Qadariyyah wamechupa mipaka katika kuthibitisha uwezo wa mja kujichagulia mwenyewe mpaka wakafikia kupinga makadirio. Wamefikia mpaka kuona kuwa mja anajitosheleza kwa matendo yake na wanayatoa nje ya utashi na matakwa ya Allaah. Kwa maana nyingine wanaona kuwa yeye ndiye ambaye anajiumbia matendo yake mwenyewe, mbali kabisa na uwezo wa Allaah. Hii ndio ´Aqiydah ya Mu´tazilah.

Kuhusu Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, wako kati na kati katika suala hili. Wanasema kuwa mja anayo matakwa na utashi na kwamba anafanya kwa kutaka kwake mwenyewe. Lakini pamoja na hivyo hatoki nje ya mipango na makadirio ya Allaah. Matendo yake yameumbwa na Allaah, lakini wakati huohuo ni matendo na machumo yake. Yeye ndiye ambaye anafanya maasi na ndiye ambaye anafanya utiifu, lakini Allaah ndiye ambaye amekadiria yale yote anayoyafanya. Kwa ajili hiyo ndio maana ima anaadhibiwa kwa makosa yake au analipwa thawabu kwa utiifu wake. Kama asingeyafanya hayo kwa kutaka kwake mwenyewe, basi asingelipwa thawabu wala kuadhibiwa. Wendawazimu, watoto na wale waliotenzwa nguvu wanaofanya mambo kwa kutokutaka kwao hawawajibiki.

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 260
  • Imechapishwa: 21/05/2025