Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

169 – Tunaona mkusanyiko ndio haki na usawa, na mgawanyiko ni upindaji na adhabu.

MAELEZO

Tunaona, Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, mkusanyiko ni haki na mgawanyiko ni adhabu. Ummah kukusanyika juu ya haki ni rehema. Kufarikiana kati yao ni adhabu. Hili ni miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Kwa hivyo ni wajibu kuwa na umoja na kuacha mifarakano. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا

“Shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja wala msifarikiane.”[1]

Kamba ya Allaah ni Qur-aan na Uislamu. Wote wanatakiwa kukusanyika juu ya Qur-aan na Sunnah. Hapa Allaah anaamrisha kukusanyika na anakataza kufarikiana. Ameeleza kuwa kukusanyika kunakuwa juu ya kamba ya Allaah – ambayo ni Qur-aan. Haijuzu kukusanyika juu ya kitu kingine, kama mfano wa mirengo na ukundikundi, kwa sababu mambo hayo yanasababisha kugawanyika. Umoja hauwi isipokuwa juu ya Kitabu cha Allaah. Allaah anaamrisha kukusanyika na kukataza kugawanyika katika fikira na nyoyo. Waislamu vyovyote hawa watakuwa mbali na hawa, wanakuwa na umoja juu ya haki. Nyoyo zao zimeshikamana na wanapendana.

Kuhusu watu wa batili, ijapo watakuwa mahali pamoja, miili yao ndio iko pamoja lakini nyoyo zao zimefarikiana. Allaah (Subha anah) amesema:

تَحْسَبُهُمْ جَمِيعًا وَقُلُوبُهُمْ شَتَّىٰ

”Utawadhania wako pamoja, kumbe nyoyo zao ziko mbalimbali.”[2]

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ تَفَرَّقُوا وَاخْتَلَفُوا مِن بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْبَيِّنَاتُ

“Wala msiwe kama wale waliofarikiana na wakatofautiana baada ya kuwajia hoja ubainifu.”[3]

وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَلَا تَكُونُوا مِنَ الْمُشْرِكِينَ مِنَ الَّذِينَ فَرَّقُوا دِينَهُمْ وَكَانُوا شِيَعًا ۖ كُلُّ حِزْبٍ بِمَا لَدَيْهِمْ فَرِحُونَ

“… na simamisheni swalah; na wala msiwe miongoni mwa washirikina. Miongoni mwa wale walioitenganisha dini yaowakawa makundi makundi. Kila kundi kwa yaliyonayo linafurahia.”[4]

شَرَعَ لَكُم مِّنَ الدِّينِ مَا وَصَّىٰ بِهِ نُوحًا وَالَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ وَمَا وَصَّيْنَا بِهِ إِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَىٰ ۖ أَنْ أَقِيمُوا الدِّينَ وَلَا تَتَفَرَّقُوا فِيهِ ۚ

“Amekuwekeeni katika dini yale aliyomuusia kwayo Nuuh na ambayo tumekuteremshia Wahy wewe na tuliyomuusia kwayo Ibraahiym na Muusa na ‘Iysaa kwamba: “Simamisheni dini na wala msifarikiane humo.”[5]

Ni wajibu kwa waislamu wawe na umoja katika ´Aqiydah yao, mkusanyiko wao na kumtii kwao mtawala wao. Waislamu wanatakiwa wawe na umoja, kama mwili na jengo moja, kama alivyopigia mfano Mtume (Swalla Allahau ´alayhi wa sallam). Hiyo ni rehema kwa waislamu. Kwa kufanya hivo zitasalimika damu zao, nyoyo zao kuungana na jamii zao kuwa na amani. Wakihakikisha haya, basi watatunukiwa riziki. Lakini wakigombana, wakapigana vita, wakakatana na wakachukiana, basi adui atawatawala ambapo baadhi watazimwanga damu za wengine.

[1] 3:103

[2] 59:14

[3] 3:105

[4] 30:31-32

[5] 42:13

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 253-255
  • Imechapishwa: 07/05/2025