19 – Mahari kuwa makubwa na gharama kubwa za sherehe za harusi ambazo zinamtia uzito yule mume

Pengine mtu akahoji kuwa hiyo ni moja miongoni mwa sababu za kuacha kuoa. Hapana. Hili pia ni sababu moja wapo ya talaka. Kivipi? Kwa sababu ya yale aliyoyatoa mume katika mahari na gharama za ndoa. Hilo humpelekea mume fikira zake kufungamana na yale madeni na pesa zile alizotoa katika ile ndoa yake. Kwa hiyo jambo lolote atalofanya yule mke lisilokuwa zuri huamsha moto wa hasira zake yule mume na akamteremshia hasira zote mke wake na hivyo akamtaliki.

Mtume mtukufu na mwenye rehema na uongofu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amependekeza uchache wa mahari na akamuombea du´aa mwenye nayo. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mwanamke mwenye baraka kubwa zaidi ni yule mwenye mahari nyepesi.”[1]

Ameipokea Ahmad na an-Nasaa´iy.

Bali Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikasirika jambo la kufanya mahari kuwa makubwa. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

”Bwana mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumweleza kuwa amemuoa mwanamke mmoja wa Answaar.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuuliza: ”Umemuoa kwa pesa ngapi?” Akajibu: ”Kwa Awaaq nne.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Kwa Awaaq nne?” Ni kana kwamba nyinyi mnachonga zile fedha kutoka katika mlima huu.”[2]

Ameipokea Imaam Muslim nayo ni Swahiyh.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikiona kikubwa kiwango hichi na ndipo akasema:

Awaaq nne?”

Ni jambo kubwa.

Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika ”Minhaaj-us-Sunnah”:

”Mtu kujitahidi kufanya mahari yakawa madogo ni Sunnah. Kwa ajili hiyo wanazuoni wamependekeza mtu asizidishe mahari ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa wake na wasichana zake. Imepokelewa kwamba ´Aliy alimpa mahari Faatwimah nguo yake ya kivita[3].”[4]

Hizi ni baadhi au miongoni mwa sababu muhimu za talaka. Kama nilivyokwambieni hatuezi kuzifanyia kikomo sababu za talaka, kwa sababu zinatofautiana kutoka nchi moja hadi nyingine, kutoka hali moja hadi nyingine.

[1] Ahmad (46/54) (25119) na an-Nasaa´iy (08/304) (9669). al-´Iraaqiy ameifanya cheni ya wapokezi wake kuwa nzuri katika ”al-Mughniy ´an Hamal-il-Asfaar” (01/386) nr. (1406).

[2] Muslim (1464).

[3] Abu Daawuud (2126).

[4] Minhaaj-us-Sunnah (04/35).

  • Mhusika: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Twalaaq – asbaabuhu wa ´ilaajuh, uk. 38-39
  • Imechapishwa: 19/04/2024