23. Mtoto ambao hawajabaleghe waamrishwe kufunga?

Swali 23: Je, mtoto ambaye yuko chini ya miaka kumi na tano anaamrishwa kufunga kama ilivyo katika jambo la swalah?

Jibu: Ndio, watoto ambao hawajabaleghe wanaamrishwa kufunga ikiwa wanaweza. Hivyo ndivo Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walivyokuwa wakifanya kwa watoto wao.

Wanachuoni wamesema kuwa msimamizi na mlezi wanatakiwa kuwaamrisha funga wale ambao wana usimamizi juu yao katika watoto kwa ajili ya kuwapa mazoezi na malezi ya misingi ya Kiislamu ndani ya nafsi zao ili ikite kwelikweli. Lakini ikiwa kunawatia uzito au kunawadhuru wasilazimishwe.

Napenda kuzindua masuala yanayofanywa na baadhi ya wazazi ambapo wanawakataza watoto kufunga tofauti na vile walivyokuwa wakifanya Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Wanadai kuwa wanawakataza watoto hawa kwa sababu ya kuwaonea huruma. Ukweli wa mambo ni kwamba kumuonea mtoto huruma kunakuwa kwa kumwamrisha nembo za Uislamu na kumzoweza nazo. Hapana shaka kwamba kufanya hivi ni katika malezi bora na ukamilifu wa uangalizi. Imethibiti kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika mwanamme ni mchunga juu ya familia yake na ataulizwa juu ya kile alichokichunga.”[1]

Kinachowapasa walezi na wasimamizi juu ya wale ambao Allaah amewabebesha jukumu juu yao katika familia na wadogo wamche Allaah (Ta´ala) juu yao na wawaamrishe zile nembo mbalimbali za Uislamu walizoamrishwa wawaamrishe.

[1] al-Bukhaariy (2409) na Muslim (1829).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: 48 mas-alatu fiy Swiyaam, uk. 23-24
  • Imechapishwa: 20/04/2021