3- Miongoni mwa matunda ya kuifikia elimu ni kuwa na matendo mema. Hakika pindi mwanafunzi atapojifunza basi matendo yake yatakuwa mema. Miongoni mwa sharti za kukubaliwa matendo na kumfuata Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), jambo ambalo halijulikani isipokuwa kwa elimu. Kwa ajili hii pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipotajiwa watu wawili ambapo mmoja wao alikuwa ni mfanya ´ibaadah na mwengine ni mwanachuoni akasema yafuatayo:

“Ubora wa mwanachuoni juu ya mfanya ´ibaadah ni kama ubora wangu juu ya mmoja wenu.” Kisha akasema: “Hakika Allaah, Malaika Wake, waliyomo mbinguni na ardhini wanamswalia yule anayewafunza watu kheri, mdudu mchungu kwenye shimo lake na hata samaki wanamswalia anayewafunza watu kheri.”[1]

Siri ya hilo ni yale waliyosema wanachuoni: mwanachuoni mfanya ´ibaadah anajua yale yanayomridhisha Allaah (´Azza wa Jall) na anayafanya na anajua yale yenye kumkasirisha Allaah (´Azza wa Jall) na anajiepusha nayo. Matokeo yake matendo yake yanakuwa sahihi na yenye kukubaliwa. Kuhusu mfanya ´ibaadah pasi na elimu anaweza kutaka kumridhisha Allaah (´Azza wa Jall) na matokeo yake akaenda kutumbukia katika kitu kinachomkasirisha. Alama ya hilo iko wazi kabisa. Ukiwatazama waislamu ambao wanamuabudu Allaah kwa ujinga utaona wanafanya mambo ya ajabu. Unaweza kumuona muislamu anataka kujikurubisha kwa Allaah (´Azza wa Jall) na kumridhisha na hivyo akaenda kulichinjia kaburi au walii na huku akidhania kuwa amefanya kitendo kikubwa. Huenda kwa kufanya hivo amechukua deni kubwa na wakati huo huo masikini huyu hajui kuwa ametumbukia katika kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

[1] at-Tirmidhiy (2685) ambaye amesema: “Ni nzuri Swahiyh na geni.” al-Albaaniy amesema: “Ni nzuri kutokana na zengine.” Tazama “Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (01/91)

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliymillaah ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Ilm wa Wasaaailuh wa Thimaaruh
  • Imechapishwa: 22/10/2016