23. Imamu na mkusanyiko wanatakiwa kusema “Aamiyn” kwa sauti

Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi anapomaliza kusoma al-Faatihah anasema kwa sauti na kwa kukokota:

“Aamiyn.”[1]

Alikuwa akiwaamrisha waswaliji kusema “Aamiyn” baada tu ya imamu kuisema na kusema:

“Pindi imamu anaposoma:

غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ وَلَا الضَّالِّينَ

“Si ya walioghadhibikiwa wala waliopotea.”[2]

semeni: “Aamiyn”. [Malaika wanasema “Aamiyn” na imamu anasema “Aamiyn”.]”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Pindi imamu anaposema “Aamiyn” na nyinyi semeni “Aamiyn”. Yule ambaye “Aamiyn” yake itaafikiana na “Aamiyn” ya Malaika basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”[3]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Pindi mmoja wenu atasema katika swalah “Aamiyn” na Malaika mbinguni wakasema “Aamiyn” na zikaafikiana, basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”

Katika Hadiyth nyingine imekuja:

“Semeni “Aamiyn” hivyo Allaah atakuitikieni.”[4]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakuna kitu ambacho mayahudi wanakuoneeni wivu kama salamu yenu na “Aamiyn” [nyuma ya imamu].”[5]

[1] al-Bukhaariy katika ”Juz’-ul-Qiraa´fah khalf al-Imaam” na Abu Daawuud kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

[2] 01:07

[3] al-Bukhaariy, Muslim, an-Nasaa’iy na ad-Daarimiy. Nyongeza imepokelewa na wengine. Katika “Fath-ul-Baariy” Haafidhw Ibn Hajar amemnasibishia nyongeza hiyo Abu Daawuud, jambo ambalo ni kosa. Nyongeza inabatilisha hoja inayotumiwa katika Hadiyth inayosema kuwa imamu hatakiwi kusema “Aamiyn”, kama ilivyopokelewa kutoka kwa Maalik. Kwa ajili hiyo amesema Haafidhw Ibn Hajar:

“Ni dalili inayofahamisha wazi ya kuwa imamu anatakiwa kusema ”Aamiyn” kwa sauti.

Kitu kinachotolea ushahidi hilo ni matamshi ya pili. Ibn ´Abdil-Barr amesema:

”Haya ndio maoni ya waislamu wengi. Mmoja wao ni Maalik kwa mujibu wa mapokezi ya wanachuoni wa al-Madiynah, kwa kuwa yamesihi kupokelewa kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallaam) kupitia kwa Abu Hurayrah na Waa-il bin Hujr.” (at-Tamhiyd (07/13)

Bi maana Hadiyth iliyoko kabla yake.

[4] Muslim na Abu ´Awaanah.

[5] al-Bukhaariy katika ”al-Adab al-Mufrad”, Ibn Maajah, Ibn Khuzaymah, Ahmad na as-Siraaj kwa isnadi mbili Swahiyh.

Faida:

Mswaliji anatakiwa kusema ”Aamiyn” kwa sauti pamoja na imamu. Wasimtangulie, kama wanavyofanya waswaliji wengi, na wala wasiiseme baada yake. Haya ndio maoni yenye nguvu niliyofikia mpaka sasa, kama nilivyoihakiki katika baadhi ya vitabu vyangu ikiwa ni pamoja na ”Silsilat-ul-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah” (952) na ”Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (01/205).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 88-89
  • Imechapishwa: 04/02/2017