Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah (Rahimahu Allaah) sade:

Amesema (Ta´ala):

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

”Kwa jina la Allaah Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.” (27:30)

رَبَّنَا وَسِعْتَ كُلَّ شَيْءٍ رَّحْمَةً وَعِلْمًا

“Mola wetu! Umekienea kila kitu kwa rehema na ujuzi!” (40:07)

وَكَانَ بِالْمُؤْمِنِينَ رَحِيمًا

“… Naye daima kwa waumini ni Mwenye kuwarehemu.” (33:43)

وَرَحْمَتِي وَسِعَتْ كُلَّ شَيْءٍ

“Rehema Yangu imeenea kila kitu.” (07:156)

كَتَبَ رَبُّكُمْ عَلَىٰ نَفْسِهِ الرَّحْمَةَ

”Mola wenu Amejikidhia Mwenyewe rehema.” (06:54)

وَهُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ

”Naye ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.” (10:107)

فَاللَّـهُ خَيْرٌ حَافِظًا ۖ وَهُوَ أَرْحَمُالرَّاحِمِينَ

”Basi Allaah ni Mbora wa kuhifadhi, Naye ni Mbora wa kurehemu kuliko wanaorehemu!” (12:64)

MAELEZO

Tunamuamini Allaah (Jalla wa ´Alaa), majina Yake mazuri na sifa Zake kuu zilizothibiti katika Qur-aan na Sunnah Swahiyh kwa njia inayolingana na Allaah. Tunafanya hivyo pasi na kupotosha, kukanusha, kuzifanyia namna na kuzilinganisha. Bali tunasema kuwa sifa Zake zote ni haki na majina Yake yote ni mazuri. Tunamthibitishia nayo Allaah kama ambavyo Yeye Mwenyewe (Jalla wa ´Alaa) amevyojithibitishia nayo, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum). Wameyathibitisha kwa njia inayolingana na Yeye. Sifa Zake hazifanani na sifa za viumbe Wake. Majina Yake hayafanani na majina ya viumbe. Yeye (Subhaanah) ana majina mazuri na yana maana kuu. Kwa ajili hii amesema:

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا

“Na Allaah ana majina mazuri kabisa; hivyo basi muombeni kwayo.” (07:180)

Hili ni kutokana na ukamilifu Wake na ukamilifu wa maana yake. Ndio maana Akayaita (Subhaanahu wa Ta´ala) kuwa ni majina mazuri kabisa.

Hakuna yeyote anayejua namna sifa Zake zilivyo isipokuwa Yeye peke yake (Subhaanahu wa Ta´ala). Anajua tofauti na tunavyojua, anahurumia tofauti na tunavyohurumia, amelingana tofauti na tunavyolingana, hushuka tofauti na tunavyoshuka, huja tofauti na tunavyokuja na hughadhibika tofauti na tunavyoghadhibika. Vivyo hivyo inahusiana na sifa nyenginezo zote:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (42:11)

Kulingana kunajulikana. Huruma inajulikana. Kughadhibika kunajulikana. Kupenda kunajulikana. Kutaka kunajulikana. Utashi unajulikana. Lakini inapokuja katika namna yake haijulikani. Hatujui namna alivyolingana. Hatujui namna anavyohurumia. Hatujui yote haya. Allaah pekee ndiye mwenye kujua haya (Subhaanahu wa Ta´ala). Lakini hata hivyo tunajua kuwa kupenda sio kuchukia, kukasirika sio kuridhia, kuridhia sio kusamehe na kadhalika. Maana ya sifa inajulikana. Lakini haya hivyo namna yake hakuna mwenye kuijua isipokuwa Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waaswitwiyyah, uk. 32-33
  • Imechapishwa: 21/10/2024