Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

167 – Tunaamini kuchomoza kwa jua upande wa magharibi na kujitokeza kwa Mnyama ardhini kutoka maeneo pake.

MAELEZO

Jua ni lenye kuendeshwa na linatembea kwa amri ya Allaah. Linachomoza mashariki na kuzama magharibi. Katika zama za mwisho, pindi kutapowadia Qiyaamah, Allaah (Subhaanah) ataliamrisha kuchomoza magharibi. Hiyo itakuwa ni alama ya Qiyaamah. Pindi litapochomoza upande wa magharibi, basi hapo Allaah hatoikubali tawbah ya mwenye kutubia. Amesema (Subhaanah):

هَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا أَن تَأْتِيَهُمُ الْمَلَائِكَةُ أَوْ يَأْتِيَ رَبُّكَ أَوْ يَأْتِيَ بَعْضُ آيَاتِ رَبِّكَ ۗ يَوْمَ يَأْتِي بَعْضُ آيَاتِ رَبِّكَ لَا يَنفَعُ نَفْسًا إِيمَانُهَا لَمْ تَكُنْ آمَنَتْ مِن قَبْلُ أَوْ كَسَبَتْ فِي إِيمَانِهَا خَيْرًا ۗ قُلِ انتَظِرُوا إِنَّا مُنتَظِرُونَ

“Je, wanangojea nini isipokuwa Malaika wawajie au awafikie Mola au ziwajie baadhi ya alama za Mola wako? Siku zitakapokuja baadhi ya alama za Mola wako haitoifaa nafsi imani yake, ikiwa haikuamini kabla, au haikuchuma katika imani yake kheri yoyote. Sema: “Ngojeeni hakika nasi tunangojea.”[1]

Hapo kafiri atasilimu, lakini Allaah hatokubali Uislamu wake. Hapo mtenda madhambi atatubia, lakini Allaah hatokubali tawbah yake.

[1] 6:158

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 247-248
  • Imechapishwa: 30/04/2025