223. Ni ipi hukumu ya kumsomea Qur-aan nzima maiti?

Swali 223: Ni ipi hukumu ya kumsomea maiti Qur-aan yote pasi na kujali mtu amefanya hivo ile siku ya saba tokea siku ya kuaga kwake dunia au mwishoni mwa mwaka? Je, maiti analipwa thawabu kwa hilo?

Jibu: Kusoma Qur-aan kwenye kaburi ni Bid´ah. Ni jambo halikupokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala kutoka kwa Maswahabah zake. Mambo yalivyo ni kwamba wakati Mtume alipokuwa akimaliza kumzika maiti anasimama karibu na kaburi na kusema:

“Muombeeni msamaha ndugu yenu na mumuombee uimara; kwani hakika hivi sasa anahojiwa.”[1]

Haya ndio ambayo yamepokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kuhusu kumsomea Qur-aan maiti kwa kutumai ya kwamba thawabu zimwendee maiti, wanazuoni wamekinzana kama thawabu hizo zinamnufaisha au hazimnufaishi? Kuna maoni mawili yaliyotangaa. Sahihi ni kwamba ni kwamba ananufaika. Hata hivyo bora ni kumuombea du´aa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anapofariki mwanadamu basi matendo yake hukatika isipokuwa mambo matatu; swadaqah yenye kuendelea, elimu ambayo watu wananufaika nayo au mtoto mwema mwenye kumuombea du´aa.”[2]

Hakutaja kisomo cha Qur-aan wala matendo mengine mema. Ingelikuwa ni miongoni mwa mambo yaliyosuniwa basi angelibainisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Isitoshe kufanya maalum kumsomea Qur-aan maiti katika siku ya saba tokea siku ya kufa kwake au mwishoni mwa mwaka ni Bid´ah. Anayefanya hivo anatakiwa kukaripiwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ninakutahadharisheni na mambo yaliyozuliwa, kwani hakika kila kilichozuliwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”[3]

[1] Abu Daawuud (3221).

[2] Muslim (1631).

[3] Abu Daawuud (4607), at-Tirmidhiy (2676) na Ibn Maajah (34). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa’” (2455).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/220-221)
  • Imechapishwa: 02/02/2026