22. Ufunguo wako wa kuingia Peponi

Hakika huo ndio ushirikina ambao Allaah (´Azza wa Jall) hatausamehe. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa, lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[1]

Dhuluma mbele ya Allaah (´Azza wa Jall) siku ya Qiyaamah ina vitabu vitatu:

1 – Kitabu ambacho Allaah hatawasamehe chochote ndani yake, nacho ni kumshirikisha Yeye. Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa pamoja Naye.

2 – Kitabu ambacho Allaah hatakiacha chochote ndani yake, nacho ni dhuluma baina ya waja ambapo baadhi yao wanawadhulumu wengine. Hakika Allaah atachukua haki yote kutoka kwa dhalimu kwenda kwa aliyedhulumiwa kikamilifu.

3 – Kitabu ambacho Allaah hakijali, nacho ni dhuluma ya mja dhidi ya nafsi yake baina yake na Mola wake (´Azza wa Jall). Hili ndicho kitabu chepesi zaidi miongoni mwa vitabu hivyo vitatu na ndilo linalofutwa kwa haraka zaidi. Huondolewa kwa kutubia, kuomba msamaha, kufanya mema yanayofuta maovu, kwa mitihani ya kufuta madhambi na mambo mengine mfano wa hayo. Tofauti na kitabu cha shirki, ambacho hakiwezi kufutwa isipokuwa kwa upwekeshaji na kitabu cha madhulumu hakiwezi kufutwa ila kwa kutoa haki kwa wenyewe waliodhulumiwa na kutaka radhi zao.

Kwa kuwa shirki ndiyo dhuluma kubwa zaidi kati ya hizo tatu mbele ya Allaah (´Azza wa Jall), basi ameharamisha Pepo kwa watu wake. Hakuna nafsi yenye shirki itakayoingia Pepo. Bali wanaoiingia ni watu wa upwekeshaji. Hakika upwekeshaji ndio ufunguo wa mlango wake. Yeyote asiye na ufunguo hatofunguliwa mlango wake. Hata akija na ufunguo ambao hauna meno, basi haingewezekana kufungua nao.

Katazo la udanganyifu, ukweli katika maneno, kutimiza amana, kuunganisha undugu wa damu na kuwafanyia wema wazazi, basi mja yeyote anayechukua katika dunia hii ufunguo sahihi wa upwekeshaji na kisha akaweka meno yake kwa kuyatekeleza yale aliyoamrishwa, basi siku ya Qiyaamah atakuja na huo ufunguo wa Pepo ambao hauwezi kufungulia isipokuwa kwao. Hakutakuwapo na kizuizi cha kumzuia asifungue, isipokuwa tu ikiwa ana madhambi, makosa na mizigo ambayo athari yake haikuondoka hapa duniani kwa kutubia na kuomba msamaha. Basi atazuiliwa kuingia Peponi mpaka atakaswe nayo. Ikiwa hali, vitisho na shida zake hazitomtakasa, basi ni lazima aingie Motoni ili kutolewa uchafu wake humo na atakaswe na uchafu wake na kinyaa chake. Kisha atatolewa humo na kuingizwa Peponi, kwani hiyo ni makaazi ya walio safi – na wala haingii ndani yake isipokuwa aliye safi. Allaah (Ta´ala) amesema:

الَّذِينَ تَتَوَفَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ طَيِّبِينَ ۙ يَقُولُونَ سَلَامٌ عَلَيْكُمُ ادْخُلُوا الْجَنَّةَ بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ

”Wale ambao Malaika wanawafisha katika hali njema watawaambia: Salaamun ‘Alaykum (amani iwe juu yenu), ingieni Jannah kwa sababu ya yale mliyokuwa mkitenda!”[2]

وَسِيقَ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ إِلَى الْجَنَّةِ زُمَرًا ۖ حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوهَا وَفُتِحَتْ أَبْوَابُهَا وَقَالَ لَهُمْ خَزَنَتُهَا سَلَامٌ عَلَيْكُمْ طِبْتُمْ فَادْخُلُوهَا خَالِدِينَ

”Na wataendeshwa wale waliomcha Mola wao kuelekea Peponi hali ya kuwa makundimakundi, mpaka watakapoifikia na ikafunguliwa milango yake, na watasema walinzi wake: “Amani iwe juu yenu furahini na ingieni hali ya kuwa ni wenye kudumu.”[3]

Kuingia kwao kumefungamanishwa na wema ambao unaashiria kuwa ndio sababu ya wao kuingia: Kutokana na sababu ya wema wenu basi mtaambiwa muingie ndani.

[1] 4:48

[2] 16:32

[3] 39:73

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 40-42
  • Imechapishwa: 05/08/2025