150 – Abu Hurayrah as-Swayrafiy ametuhadithia: Abu Twulayq – ambaye alikuwa mtu mwema – ametuhadithia: Mu´aadh bin Hishaam ametuhadithia: Baba yangu ametuhadithia, kutoka kwa Qataadah, kutoka kwa Abu Swaalih, ambaye amesema:

”Salman alikuwa akiweka mkono wa nguo yake juu ya kifundo cha mkono na kanzu yake hadi magotini.”

151 – Muhammad bin ´Abbaad amenihadithia: Zayd bin al-Hubaab ametuhadithia: Mu´aawiyah bin Swaalih ametuhadithia: Sa´iyd bin Suwayd – mmoja katika walinzi wa ´Umar bin ´Abdil-´Aziyz – amenihadithia:

”´Umar bin ´Abdil-´Aziyz alituswalisha swalah ya ijumaa, kisha akaketi chini. Alikuwa amevaa kanzu iliyoshonwa sehemu ya mbele na nyuma. Mtu mmoja akamwambia: “Ee kiongozi wa Waumini! Hakika Allaah (´Azza wa Jall)  amekupa –kwa nini huvai kitu bora?” Akainamisha kichwa kwa muda mrefu hadi tukajua kuwa maneno hayo yamemchukiza. Halafu akainua kichwa chake na kusema: ”Hakika ya wastani bora zaidi ni wakati wa kuwa na mali, na msamaha bora zaidi ni wakati wa uwezo.”

152 – ´Ubaydullaah bin ´Umar al-Jushamiy ametuhadithia: Haramiy bin ´Imaarah ametuhadithia, kutoka kwa Shu´bah, kutoka kwa Qataadah, kutoka kwa Sa´iyd bin al-Musayyab, ambaye amesema:

“Tengeneza moyo wako, kisha vaa upendavyo.”

153 – Haaruun bin ´Abdillaah ametuhadithia: Ma´n bin ´Iysaa ametuhadithia: Nimewasikia baadhi ya wanazuoni wakisema kwamba ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Enyi wana wa israaiyl, mbona mnanijia mkiwa mmevaa mavazi ya watawa lakini mioyo yenu ni mioyo ya mbwa mwitu wenye njaa? Vaeni mavazi ya wafalme na lainisheni mioyo yenu kwa kumwogopa Allaah.”

154 – ´Abdur-Rahmaan bin Swaalih amenihadithia: al-Muhaaribiy ametuhadithia, kutoka kwa ´Ubaydullaah bin al-Waliyd, kutoka kwa Fudhwayl bin Muslim, kutoka kwa baba yake – ambaye alikuwa akiuza mashati karibu na nyumba ya Furaat huko Kuufah – amesema:

”´Aliy bin Abiy Twaalib alisimama mbele yetu na akasema: ”[…] shati hili.” Akalivaa kisha akasema: ”Shati hili ni kwa bei gani?” Akaambiwa: ”Kwa dirhamu tatu, ee kiongozi wa Waumini!” Akanyoosha mkono wake na shati likawa linazidi vidole vyake, akasema: ”Likate mpaka mwisho wa vidole vyangu, kisha akasema: Lifunge.” Nikasema: ”Naliweke upindo?” Akasema: ”Ndio, iwapo kufunga huko ni kuweka upindo basi liweke upindo.” Kisha akainua shati lake na kutoa katika mfuko wake dirhamu tatu, kisha akaondoka huku akisema: ”Inatosha kikufikishacho mahali.” Shati hilo lilikuwa ni la kitani.”

155 – Abu Hurayrah as-Swayrafiy ametukhabarisha: Abu Twulayq – ambaye alikuwa mtu mwema – amenihadithia: Mu´aadh bin Hishaam ametuhadithia: Baba yangu amenihadithia, kutoka kwa Budayl, kutoka kwa Shihr bin Hawshab, kutoka kwa Asmaa’, aliyesema:

”Urefu wa mkono wa shati la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ulikuwa chini kidogo ya kifundo cha mkono.”[1]

156 – al-Hasan bin Yahyaa ametuhadithia: Haazim bin Jabalah ametuhadithia, kutoka kwa Ibraahiym bin Adham, kutoka kwa Ibraahiym, kutok kwa ´Ikrimah, kutoka kwa Ibn ´Abbaas, aliyesimulia kwamba Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Anayeacha mapambo ya Allaah (´Azza wa Jall) au akaweka chini nguo nzuri kwa kunyenyekea kwa ajili ya Allaah (´Azza wa Jall) na kutafuta uso Wake, ni haki juu ya Allaah (´Azza wa Jall) kumhifadhia mazulia bora ya Peponi katika vitanda vya yakuti.”

[1] Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “adh-Dhwa´iyfah” (3457).

  • Muhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa (afk. 281)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Khumuul wat-Tawaadhwu´, uk. 190-198
  • Imechapishwa: 24/03/2026