Hakuna tafsiri miongoni mwa tafsiri zao batili isipokuwa batili yake inaonekana kwa njia nyingi, wakati fulani kwa kujua ubatili wa ´Aqiydah yao na mara nyingine kwa kujua ubatili wa tafsiri waliyoitumia kwa Qur-aan, ima iwe ni hoja kwa ´Aqiydah yao au jibu kwa waliowapinga. Miongoni mwao kuna wale wenye ufaswaha na maneno mazuri, lakini huingiza Bid´ah ndani ya maneno yake, kwa sababu wengi wa watu hawaelewi hilo. Mmoja katika watu hao ni ”al-Kashshaf”, kiasi cha kwamba husambaza tafsiri zao batili kwa watu wengi ambao hawaamini batili hizo kabisa. Nimewaona wanazuoni wa tafsiri wengi wakinakili tafsiri zao, ndani ya vitabu na maneno yao, yale mambo ambayo yanaenda sambamba na ´Aqiydah zao na ambayo ima wanajua au wanaitakidi kuwa ni batili, bila ya wao kulihisi hilo. Kwa sababu ya kupindukia kwao na upotovu wao baadaye wamewafungulia njia Raafidhwah Imaamiyyah, kisha wanafalsafa na halafu Qaraamitwah na wengineo ambao walihusika katika mambo mabaya zaidi kuliko haya.

Na hali ikazidi kuwa mbaya kwa wanafalsafa, Qaraaamitwah na Raafidhwah, kwa sababu wamefasiri Qur-aan kwa njia ambazo huacha wanazuoni wakiwa na mshangao mkubwa. Kwa mfano Raafidhwah wamefasiri:

تَبَّتْ يَدَا أَبِي لَهَبٍ وَتَبَّ

“Imeteketea mikono miwili ya Abu Lahab!”[1]

kwamba inamkusudia Abu Bakr na ´Umar. Wanasema:

لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ

“… Ukifanya shirki bila shaka yataporomoka matendo yako… ”[2]

kwamba inahusu uchaguzi kati ya Abu Bakr, ´Umar na ´Aliy juu ya ukhaliyfah. Wanasema kwamba:

إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُكُمْ أَن تَذْبَحُوا بَقَرَةً

”Hakika Allaah anakuamuruni mchinje ng’ombe.”[3]

inamkusudia ´Aaishah. Wanasema kwamba:

فَقَاتِلُوا أَئِمَّةَ الْكُفْرِ

“… basi wapigeni vita viongozi wa ukafiri… ”[4]

inamkusudia Twalhah na az-Zubayr. Wanasema kwamba:

مَرَجَ الْبَحْرَيْنِ يَلْتَقِيَانِ

”Ameziachilia bahari mbili zinakutana.”[5]

inamkusudia ´Aliy na Faatwimah. Wanasema kwamba:

يَخْرُجُ مِنْهُمَا اللُّؤْلُؤُ وَالْمَرْجَانُ

”Zinatoka humo lulu na marijani.”[6]

 inamkusudia al-Hasan na al-Husayn. Wanasema kwamba:

وَكُلَّ شَيْءٍ أَحْصَيْنَاهُ فِي إِمَامٍ مُّبِينٍ

“Kila kitu Tumekirekodi barabara katika kitabu kinachobainisha.”[7]

inamkusudia ´Aliy bin Abiy Twaalib. Wanasema kwamba:

عَمَّ يَتَسَاءَلُونَ عَنِ النَّبَإِ الْعَظِيمِ

”Kuhusu nini wanaulizana? Kuhusu khabari kubwa mno ya muhimu… ”[8]

inamkusudia ´Aliy bin Abiy Twaalib. Wanasema kwamba:

إِنَّمَا وَلِيُّكُمُ اللَّـهُ وَرَسُولُهُ وَالَّذِينَ آمَنُوا الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَهُمْ رَاكِعُونَ

”Hakika si vyenginevyo Mlinzi wenu ni Allaah na Mtume Wake na wale walioamini, ambao wanasimamisha swalah na wanatoa zakaah hali ya kuwa wananyenyekea.”[9]

inamkusudia ´Aliy. Isitoshe hutaja Hadiyth iliyotungwa kwa maafikiano ya wanazuoni wote, nayo ni kule kutoa kwake swadaqah akiwa ndani ya swalah. Wanasema kwamba:

أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ

”Hao zitakuwa juu yao sifa kutoka kwa Mola wao na rehemana – hao ndio wenye kuongoka.”[10]

imeteremshwa juu ya ´Aliy wakati alipouliwa Hamzah.

[1] 111:1

[2] 39:65

[3] 2:67

[4] 9:12

[5] 55:19

[6] 55:22

[7] 36:12

[8] 78:1-2

[9] 5:55

[10] 2:157

  • Muhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Muqaddimah fiy Usuwl-it-Tafsiyr, uk. 76-78
  • Imechapishwa: 03/04/2025