Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:
163 – Wanazuoni wa Salaf katika wale waliotangulia na wa baada yao katika wale waliokuja baadaye ambao ni watu wema waliokuwa wanafata mapokezi na waliokuwa na ufahamu na uoni, haitakiw kuwataja isipokuwa kwa njia nzuri tu. Yule mwenye kuwataja kwa ubaya hafuati njia ya sawa.
MAELEZO
Alipomaliza kutaja haki za Maswahabah na watu wa nyumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), yale mapenzi yanayopasa juu yao na kutomtukana yeyote katika wao, ndipo akaenda (Rahimahu Allaah) kwa wale wanaofuata katika ubora; nao ni wanazuoni. Wanazuoni wa ummah wana nafasi na ubora baada ya Maswahabah. Kwa sababu wanazuoni ndio warithi wa Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
“Wanazuoni ndio warithi wa Mitume. Hakika Mitume hawakuacha dinari wala dirhamu, hakika si vyenginevyo walichoacha ni elimu. Yule mwenye kujinyakulia nayo basi amebeba fungu kubwa.”[1]
Wanaokusudiwa ni wanazuoni wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, wanazuoni walio na uoni na uelewa na wanaofata mapokezi. Nao kwa msemo mwingine ni Ahl-ul-Hadiyth.
Wanazuoni wamegawanyika sampuli mbili:
1 – Wanazuoni wa mapokezi (الأثر). Wanazuoni wa Hadiyth. Ni wale wanaotilia umuhimu Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam), wakazihifadhi, wakazitetea na wakawafikishia nazo ummah zikiwa safi kabisa, kama alivyozitamka Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Wakazikinga na kila kisichostahiki kuingia na kila uwongo na wakazitenga na Hadiyth zilizozuliwa, wakazibainisha na kuzitambulisho. Hawa ndio wanazuoni wa masimulizi (علماء الرواية).
2 – Wanazuoni wa Fiqh. Hawa ni wale wanazuoni ambao wananyofoa hukumu mbalimbali kutoka katika dalili hizi, wakabainisha uelewa wake, wakazisherehesha na kuwabainishia nazo watu. Hawa ndio wanazuoni wa elimu inayosimuliwa (علماء الدراية).
Baadhi ya wanazuoni wamekusanya aina zote mbili, akiwemo Imaam Ahmad, Maalik, ash-Shaafi´iy na al-Bukhaariy. Wanazuoni wote hawa wana fadhilah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) amesema:
“Allaah ampambe mtu ambaye amesikia maneno yangu, akayahifadhi, akayaelewa na kuyafikisha kama alivyoyasikia.”[2]
Mtume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) amewaombea du´aa na kuwasifu. Wanazuoni wamesimamia majukumu waliyopewa na Allaah katika kuitetea dini na ´Aqiydah. Wanazibainisha hukumu, mirathi, yaliyo halali na yaliyo haramu na maana ya Qur-aan na Sunnah. Wamewaachia ummah hazina kubwa ambayo wanafaidika nayo na kurejea katika vipimo wakati mambo yanapotatiza.
Uelewa umegawanyika sampuli mbili:
1 – Uelewa mkubwa, bi maana ule uelewa wa ´Aqiydah.
2 – Uelewa wa kuzitendea kazi hukumu. Si muhimu zaidi kuliko uelewa mkubwa.
Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema wakati alipokuwa anasisitiza ubora wa wanazuoni:
“Ubora wa mwanachuoni ukimlinganisha na mfanya ´ibaadah ni kama ubora wa nyota ukilinganisha na sayari zilizosalia.”[3]
Hilo ni kwa sababu manufaa yao yanaenea. Imekuja katika upokezi mwingine:
“Ubora wa mwanachuoni ukimlinganisha na mfanya ´ibaadah ni kama ubora wangu ukilinganisha na yule aliye chini yenu kabisa.”[4]
Wanazuoni wana haki ya kuheshimiwa na wana hadhi. Kwa hivyo haijuzu kuwaponda na kuwadharau hata kama kutatokea kwa baadhi yao makosa katika mambo ya kujitahidi. Makosa kama haya ya kujitahidi hayapelekei kuwadharau. Wanaweza kukosea licha ya kwamba wamekusudia haki. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
“Anapojitahidi hakimu na akapatia, basi ana ujira mara mbili. Na anapojitahidi na akakosea, basi ana ujira mara moja.”[5]
Hadiyth hii inawahusu wanazuoni na si wale wanaojifanya na wao ni wanazuoni. Wanaojifanya ni wanazuoni hawana haki kabisa ya kuingia katika mambo wasiyoyaweza.
[1]Abu Daawuud (463), at-Tirmidhiy (2687) na Ibn Maajah (223). Nzuri kupitia zingine kwa mujibu wa al-Albaaniykatika ”Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (70).
[2]Ibn Maajah (230-232) na (3056). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniykatika ”Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (91).
[3]at-Tirmidhiy (2682). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniykatika ”Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy” (2682).
[4]at-Tirmidhiy (2685). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniykatika ”Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy” (2685).
[5]al-Bukhaariy (6919) na Muslim (1716).
- Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 236-238
- Imechapishwa: 28/04/2025
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)