Ni lazima kuwapenda Maswahabah wote. Hatuingilii vile vita vilivyotokea kati yao. Vile vita vilivyotokea kati yao ni kutokana na kufasiri kwao kimakosa. Walikuwa ni wenye kujitahidi kuifikia haki. Ambaye alipatia katika wao anapata thawabu mara mbili, na ambaye amekosea katika wao anapata thawabu mara moja. Aidha wana mema na mambo mengine ya fadhilah ambayo yanafuta yale makosa yanayowatokea. Kwa ajili hiyo ni lazima kwa waislamu kuwa radhi nao, kuwapa udhuru na kuwatetea. ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kwmaba hawaingilii yale magomvi yaliyotokea kati ya Maswahabah kutokana na ubora walionao na kutangulia kwao. Jengine Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msiwatukane Maswahabah wangu. Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi ya Muhammad imo mikononi Mwake lau mmoja wenu atajitolea dhahabu mfano wa mlima wa Uhud basi hatofikia viganja viwili vya mikono vilivyojazwa na mmoja wao wala nusu yake.”[1]

Hilo kama tulivosema ni kutokana na ubora wao. Yule ambaye ataingilia yale yaliyotokea kati ya Maswahabah na hivyo kukaingia moyoni mwake chuki dhidi yao, basi huyo ni mzandiki. Kuhusu ambaye atasema kuwa anaingilia yale yaliyotokea kati yao kwa lengo la kutafiti, hiyo ni khatari kubwa na haijuzu. Wakati ´Umar bin ´Abdil-´Aziyz (Rahimahu Allaah) alipoulizwa kuhusu mizozo ya Maswahabah, alisema:

“Hao ni watu ambao ameisafisha mikono yetu kutokana na damu zao. Kwa ajili hiyo tunalazimika kuzisafisha ndimi zetu kutokana na heshima zao.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hebu si mniachie Maswahabah zangu?”[2]

Kwa hivyo hatuingilii yale yaliyotokea kati ya Maswahabah. Kwa sababu hivo ndivo inavopelekea imani. Hivo ndivo inavopelekea kumtakia mema Allaah, Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Kitabu Chake na waislamu wote kwa jumla na wale watu wao maalum.

[1]al-Bukhaariy (3673) na Muslim (2540).

[2]Ahmad katika ”Fadhwaa-il-us-Swahaabah” (297) na al-Bukhaariy (3661).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 229-230
  • Imechapishwa: 23/04/2025