21. Mwenye hedhi na nifasi wanaruhusiwa kutofunga Ramadhaan

3 – Mwanamke mwenye hedhi na mwenye damu ya uzazi ni haramu kwao kufunga katika kipindi cha hedhi na nifasi. Hii ni kwa mujibu wa yaliyo ndani ya al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesema:

”Tulikuwa tunaamrishwa kulipa swawm.” Hapo ni pale alipoulizwa: ”Kwa nini mwenye hedhi analipa swawm lakini halipi swalah?” Akasema: ”Tulikuwa tunaamrishwa kulipa swawm wala hatukuamrishwa kulipa swalah.”[1]

Na ni haramu kwa mwenye hedhi kufunga wakati wa hedhi kwa maafikiano ya wanazuoni.

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

”Imethibiti kwa mujibu wa Sunnah na kwa maafikiano ya waislamu kwamba hedhi inapingana na swawm. Kwa hivyo haijuzu swawm pamoja na hedhi au damu ya uzazi. Yeyote kati yao atakayefunga katika hali hiyo, basi swawm yake haisihi.”

Akasema:

”Na hili linaafikiana na kipimo, kwani Shari´ah imekuja kwa uadilifu katika kila jambo. Kufunga wakati wa kutoka damu kunasababisha upungufu wa mwili na udhaifu na kunaitoa swawm katika hali ya wastani. Kwa hiyo wakaamrishwa kufunga nje ya nyakati za hedhi ili swawm yao iwe ni swawm ya wastani isiyotoka damu inayoupa mwili nguvu ambayo ndiyo msingi wake, tofauti na mwenye damu ya ugonjwa. Mwenye kutapika kwa kushindwa kujizuia, kwa kuwa mambo hayo hayana wakati maalum unaoweza kuepukwa, hivyo hayakufanywa kuwa yanayobatilisha swawm.”

[1] al-Bukhaariy (321) na Muslim (69/335).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithaaf Ahl-il-Iymaan bi Duruus Shahri Ramadhwaan, uk. 27
  • Imechapishwa: 12/02/2026