Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَلَوْلَا إِذْ دَخَلْتَ جَنَّتَكَ قُلْتَ مَا شَاءَ اللَّـهُ لَا قُوَّةَ إِلَّا بِاللَّـهِ

“Na lau ulipoingia bustanini mwako ungelisema: “Ametaka Allaah; hapana nguvu isipokuwa kwa Allaah.” (18:39)

وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا اقْتَتَلُوا وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَفْعَلُ مَا يُرِيدُ

“Na lau Angelitaka Allaah wasingelipigana; lakini Allaah anafanya ayatakayo.” (02:153)

إِنَّ اللَّـهَ يَحْكُمُ مَا يُرِيدُ

”Hakika Allaah anahukumu atakayo.” (05:01)

فَمَن يُرِدِ اللَّـهُ أَن يَهْدِيَهُ يَشْرَحْ صَدْرَهُ لِلْإِسْلَامِ ۖ وَمَن يُرِدْ أَن يُضِلَّهُ يَجْعَلْ صَدْرَهُ ضَيِّقًا حَرَجًا كَأَنَّمَا يَصَّعَّدُ فِي السَّمَاءِ

”Basi yule ambaye Allaah Anataka kumwongoza, Humfungulia kifua chake kwa Uislamu, na yule ambaye anataka kumpoteza humjaalia kifua chake kuwa na dhiki chenye kubana kama kwamba anapanda mbinguni kwa tabu.” (06:125)

MAELEZO

Vilevile Allaah anasifika kuwa na matakwa. Maana yake ni utashi wa kilimwengu. Kwa msemo mwingine matakwa Yake ni yenye kutendeka na hayazuiwi na kitu. Kile anachotaka Allaah ndio huwa, ni mamoja iwe ni mauti, uhai, kuwafanya watu fulani wawe na nguvu, kuwafanya watu wengine wawe madhalili, kuwaondoshea watu fulani ufalme, kuwafanya watu fulani wawe na ufalme, kuwafanya watu fulani wapate watoto au kutowapata. Yote hayo ni yenye kutendeka pale Allaah anapotaka. Amesema (Ta´ala):

لِمَن شَاءَ مِنكُمْ أَن يَسْتَقِيمَ وَمَا تَشَاءُونَ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

“Kwa yule atakaye miongoni mwenu anyooke. Na hamtotaka isipokuwa atake Allaah, Mola wa walimwengu.” (81:28-29)

وَلَوْ شَاءَ رَبُّكَ مَا فَعَلُوهُ

“Na lau angetaka Mola wako wasingeliyafanya hayo.” (06:112)

وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا اقْتَتَلُوا

“Na lau angelitaka Allaah wasingelipigana.” (02:253)

وَهُوَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ

”Naye ndiye Mjuzi, Mwenye hekima.” (66:02)

عْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ وَأَنَّ اللَّـهَ قَدْ أَحَاطَ بِكُلِّ شَيْءٍ عِلْمًا

”Ili mjue kwamba Allaah juu ya jambo ni Muweza na kwamba Allaah amekwishakizunguka kila kitu kwa ujuzi.” (65:12)

Vilevile Aayah nyenginezo ambazo zimetaja Ujuzi na hekima. Kwa mfano:

إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

“Hakika Allaah ni Mshindi, Mwenye hekima.” (02:220)

Kuna aina mbili za utashi:

1 – Utashi wa kilimwengu (Kawniyyah). Utashi wa kilimwengu ni matakwa. Utashi aina hii ni wenye kutekelezwa na haurudishwi na kitu. Mfano wa maneno Yake (Ta´ala):

فَمَن يُرِدِ اللَّـهُ أَن يَهْدِيَهُ يَشْرَحْ صَدْرَهُ لِلْإِسْلَامِ ۖ وَمَن يُرِدْ أَن يُضِلَّهُ يَجْعَلْ صَدْرَهُ ضَيِّقًا حَرَجًا كَأَنَّمَا يَصَّعَّدُ فِي السَّمَاءِ

”Basi yule ambaye Allaah Anataka kumwongoza, humfungulia kifua chake kwa Uislamu, na yule ambaye anataka kumpoteza humjaalia kifua chake kuwa na dhiki chenye kubana kama kwamba anapanda mbinguni kwa tabu.” (06:125)

إِنَّ اللَّـهَ يَحْكُمُ مَا يُرِيدُ

“Hakika Allaah anahukumu atakayo.” (05:01)

Huu ni utashi wa kilimwengu wenye kutendeka. Ni kama mfano wa matakwa. Haurudishwi na kitu.

2 – Utashi wa kidini (Shar´iyyah). Utashi aina hii maana yake ni kupenda na kuridhia. Utashi huu unaweza kutokea na huenda vilevile usitokee. Mfano wa maneno Yake (Ta´ala):

يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُبَيِّنَ لَكُمْ وَيَهْدِيَكُمْ سُنَنَ الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ وَيَتُوبَ عَلَيْكُمْ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ وَاللَّـهُ يُرِيدُ أَن يَتُوبَ عَلَيْكُمْ

“Allaah anataka kukubainishieni na kukuongozeni nyendo za wale walio kabla yenu na apokee tawbah kwenu. Na Allaah ni Mjuzi, Mwenye hekima. Na Allaah anataka kupokea tawbah kwenu.” (04:26-27)

Huu ni utashi wa kidini ambao unaweza kutokea kama ambavyo vilevile huenda usitokee. Allaah anapenda awaongoze waislamu wote. Allaah anapenda awasamehe. Huu ni utashi wa kidini. Viumbe wengi hawakusamehewa. Viumbe wengi wamekufa juu ya kufuru. Utashi wa kidini unaweza kutokea kama ambavyo vilevile huenda usitokee.

Allaah amependa kidini wanaadamu wakubali haki, wawafuate Mitume na wamtii Allaah. Pamoja na hivyo wako miongoni mwao ambao wamemtii na wengine wakamuasi. Mwenye kumtii ana Pepo, na mwenye kumuasi ana Moto. Amesema (Jalla wa ´Alaa):

تِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ ۚ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ يُدْخِلْهُ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ وَذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَيَتَعَدَّ حُدُودَهُ يُدْخِلْهُ نَارًا خَالِدًا فِيهَا وَلَهُ عَذَابٌ مُّهِينٌ

“Hiyo ni mipaka ya Allaah. Na yeyote atakayemtii Allaah na Mtume Wake atamwingiza katika Pepo zipitazo chini yake mito, ni wenye kudumu humo, na huko ndiko kufuzu kukubwa kabisa. Na yeyote atakayemuasi Allaah na Mtume Wake na akapindukia mipaka Yake atamwingiza Motoni, ni mwenye kudumu humo na atapata adhabu ya kudhalilisha.” (04:13-14)

Wote wamepewa matishio ya adhabu. Mwenye kutii kwa khiyari na kutaka kwake basi ana Pepo. Na yule mwenye kuasi ana Moto. Huu ni utashi wa kidini.

Kuhusiana na utashi wa kilimwengu hakuna yeyote anaweza kuukwepa. Yale anayotaka Allaah yatokee katika ulimwengu ni lazima yatokee. Kwa mfano Allaah anapotaka kuwaangamiza watu fulani, kuwafanya wawe na utukufu, kumfisha fulani, kumpa uhai, kumhuisha fulani, kumfanya akaishi na mengineyo. Utashi wa kilimwengu ni kama mfano wa matakwa. Matakwa yake ni lazima yatendeke.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 29-30
  • Imechapishwa: 19/10/2024