Yaziyd bin Haaruun amesimulia katika kikao chake kutoka kwa Ismaa´iyil bin Abiy Khaalid, kutoka kwa Qays bin Abiy Haazim, kutoka kwa Jariyr bin ´Abdillaah, ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuhusu Uonekanaji:

”Hakika nyinyi mtamuona Mola wenu kama mnavyouona mwezi usiku wa mwezi mng´aro.”

Bwana mmoja akasema katika kikao chake: ”Ee Abu Khaalid! Nini maana ya Hadiyth?” Akaghadhibika na kukerwa na kusema: ”Unafanana na Swabiygh! Unahitaji kile kilichomkuta! Maangamivu ni yako! Ni nani anayejua itakuwa namna gani? Hakuna anayefanya hivo isipokuwa tu mtenda dhambi, ambaye anaichukulia wepesi dini yake. Unaposikia Hadiyth kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi ifuate na wala usizue kitu juu yake. Kwani hakika nyinyi mkiifuata na msigombane juu yake, basi mtasalimika. Msipoyafanya hayo, mtaangamia.”

Kisa cha Swabiygh, ambacho Yaziyd bin Haaruun amekitaja kama mfano kwa muulizaji, amekisimulia Yahyaa bin Sa´iyd, kutoka kwa Sa´iyd bin al-Musayyab, aliyesema:

Swabiygh alimwendea Kiongozi wa waumini ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) na kusema: ”Ee Kiongozi wa waumini! Nieleze kuhusu:

وَالذَّارِيَاتِ ذَرْوًا

“Ninaapa kwa pepo zinazotawanya… ”[1]

Akasema: ”Ni pepo. Kama nisingelimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema hivo, basi katu nisingelisema hivo.” Akasema: ”Nieleze kuhusu:

فَالْحَامِلَاتِ وِقْرًا

”… ninaapa kwa mawingu yanayobeba mzigo… ”[2]

Akasema: ”Ni mawingu. Kama nisingelimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema hivo, basi katu nisingelisema hivo.” Akasema: ”Nieleze kuhusu:

فَالْمُقَسِّمَاتِ أَمْرًا

”… kisha Naapa kwa wenye kugawanya amri!”[3]

Akasema: ”Ni Malaika. Kama nisingelimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema hivo, basi katu nisingelisema hivo.” Akasema: ”Nieleze kuhusu:

فَالْجَارِيَاتِ يُسْرًا

”… kisha naapa kwa zinazotembea kwa wepesi… ”[4]

Akasema: ”Ni marikebu. Kama nisingelimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema hivo, basi katu nisingelisema hivo.” Kisha akaamrisha akapigwa bakora mia moja na kuwekwa chini ya kizuizi cha nyumbani. Baada ya kupata nafuu, akaamrishwa akapigwa viboko mia moja vingine halafu akafukuzwa kwenye tandiko ndogo la ngamia. Akamwandikia Abu Muusa al-Ash´ariy: ”Ni marufuku kwake kukaa na watu.” Akabaki katika hali hiyo mpaka alipopelekwa kwa Abu Muusa al-Ash´ariy na akaapa viapo vikubwa ya kwamba hahisi tena chochote ndani ya nafsi yake yale aliyokuwa akiyahisi hapo kabla. Akamwandikia ´Umar na kumweleza. Akamwandikia kumjibu: ”Nadhani kuwa ni msema kweli. Mwache akae na watu.”

Hammaad bin Zayd amesimulia kutoka kwa Qutwn bin Ka´b: Nimemsikia bwana mmoja kutoka katika Banuu ´Ijl kwa jina Khaalid bin Zur´ah akihadithia kutoka kwa baba yake, ambaye amesema:

”Nimemuona Swabiygh huko Baswrah. Utasema ni ngamia mwenye ugonjwa. Alikuwa akija kwenye mkusanyiko wa watu. Pale tu anapoketi kati ya watu wasiomjua, basi anaita kwa sauti bwana mwingine kutoka kwenye mkusanyiko mwingine: ”Amri ya Kiongozi wa waumini!”

Hammaad bin Zayd vilevile amesimulia kutoka kwa Yaziyd bin Haazim, kutoka kwa Sulaymaan bin Yasaar, ambaye amesema:

”Bwana mmoja kutoka katika Banuu Tamiym alifika Madiynah. Alikuwa na vitabu na akawa anauliza kuhusu Aayah za Qur-aan zisizokuwa wazi.  ´Umar akafikiwa na khabari hiyo, akamtumia mjumbe. Wakati huohuo alikuwa amemwandalia mabua ya mtende. Alipoingia kwake, akaketi chini. Akasema: ”Wewe ni nani?” Akasema: ”Mimi ni mja wa Allaah Swabiygh.” Akasema: ”Na mimi pia ni mja wa Allaah ´Umar.” Kisha akamsogelea na kuanza kumpiga na yale mabua ya mtende. Akaendelea kumpiga mpaka akamuumiza. Damu ikaanza kutiririka usoni mwake, akasema: ”Tosha, ee Kiongozi wa waumini! Naapa kwa Allaah yameniondoka yale niliyokuwa nahisi kichwani mwangu!”

[1] 51:1

[2] 51:2

[3] 51:4

[4] 51:3

  • Mhusika: Imaam Abu ´Uthmaan Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Swaabuuniy (afk. 449)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth, uk. 236-242
  • Imechapishwa: 11/12/2023