01. Tambua kuwa Uislamu ndio Sunnah na Sunnah ndio Uislamu

Imaam al-Barbahaariy (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Tambua kuwa Uislamu ndio Sunnah na Sunnah ndio Uislamu na kimoja katika hayo hakisimami isipokuwa kwa kingine.

Uislamu ni njia waliyokuja nayo Mitume (´alayhimus-Swalaatu was-Salaam). Mitume wote walikuja na Uislamu. Kila Mtume aliyelingania katika dini ya Allaah na akaja na Shari´ah kutoka kwa Allaah, basi huo ndio Uislamu.

Uislamu ni kumuabudu Allaah (´Azza wa Jall) katika kila wakati kwa yale aliyoyaweka katika Shari´ah. Aliyoyaweka katika kila wakati. Allaah amewawekea Mitume mambo ya Shari´ah kwa muda fulani kisha anayafuta. Pindi Anapofuta ile iliyokuja kufuta ndio inakuwa Uislamu mpaka ilipokuja Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Jalla wa ´Alaa) Anasema:

لِكُلِّ أَجَلٍ كِتَابٌ  يَمْحُو اللَّـهُ مَا يَشَاءُ وَيُثْبِتُ ۖ وَعِندَهُ أُمُّ الْكِتَابِ

“Kwa kila kipindi kina hukmu. Allaah Anafuta na Anathibitisha yale Ayatakayo na Kwake ndiko kuna Mama wa Kitabu.” (13:38-39)

Uislamu ni yale malinganizi na matendo yaliyokuja na Mitume. Kila wakati na yanayoendana na wakati huo. Hali iliendelea kuwa hivyo mpaka alipotumwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ukawa Uislamu ni yale aliyokuja nayo na si vinginevyo. Yule mwenye kubaki katika dini zilizotangulia na asimuamini Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi huyo sio Muislamu. Bi maana hakujisalimisha kwa Allaah (´Azza wa Jall) na kumtii Mtume huyu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu aliyokuwemo yameisha na kufutwa. Kubaki katika kitu kilichofutwa sio dini ya Allaah (´Azza wa Jall). Kutendea kazi kile kilichokuja kufuta ndio dini.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Sharh-is-Sunnah, uk. 13
  • Imechapishwa: 13/06/2017