Allaah (´Azza wa Jall) ameahidi kumuitikia yule mwenye kumuomba. Pengine mtu akasema kuwa ameomba lakini hakuitikiwa. Kikwazo kitakuwa kwako. Du´aa ni sababu tu miongoni mwa sababu. Natija haipatikani isipokuwa kunapoondoka vikwazo. Pengine kizuizi ni kwamba umeomba hali ya kuwa na moyo wenye kughafilika na pasi na mazingatio; ni vipi basi ataitikiwa mtu mwenye moyo ulioghafilika na asiyekuwa na mazingatio? Huenda unakula haramu, unakunywa haramu na unavaa haramu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nywele zake timtim na miguu yake imejaa vumbi. Ananyanyua mikono yake kuelekea mbinguni na anasema: “Ee Mola! Ee Mola!” Lakini chakula chake ni haramu, mavazi yake ni haramu na amekulia katika haramu; ni vipi ataitikiwa?”[1]

Au pengine anaomba jambo lenye dhambi au kukata kizazi. Hawezi kuitikiwa. Hili ni mosi.

Sababu nyingine ni kwamba Allaah (´Azza wa Jall) ni mtambuzi zaidi wa yale ambayo ni mazuri zaidi kwako.Wakati fulani anaweza kuharakisha kukuitikia na wakati mwingine anaweza kuchelewesha. Anaweza vilevile kukukinga kutokana na ovu linalolingana na du´aa yako, pasi na wewe kujua jambo hilo. Kama ilivyokuja katika Hadiyth:

“Hakuna mtu ambaye anamuomba Allaah maombi isipokuwa huitikiwa. Ima akaharakishiwa ulimwengu au akawekewa nayo huko Aakhirah au akasamehewa madhambi yake kwa kiasi cha kile alichoomba – muda wa kuwa hajaomba kitu chenye dhambi au kukata kizazi au akafanya haraka.” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni vipi atafanya haraka?” Akasema: “Husema: “Nimemuomba Allaah, lakini hakuniitikia.”[2]

Wapotofu wanasema kuwa hapana haja ya kuomba du´aa. Wanajengea hoja yao eti ikiwa jambo limekwishakadiriwa kulipata, basi hapana maana yoyote ya kuomba du´aa – utakipata kwa hali yoyote hata kama hukuomba du´aa. Na kama hicho unachokiomba hujakadiriwa nacho, unaomba kitu ambacho hutopata. Fikira hii ni upotofu na inaenda kinyume na maneno ya Allaah (´Azza wa Jall). Ukweli wa mambo ni kwamba hakuna kugongana kati ya kuomba du´aa na makadirio na mipango. Ambaye amepanga na kukadiria ndiye ambaye ameamrisha kuomba du´aa. Du´aa ni sababu tu miongoni mwa sababu, lakini Allaah (´Azza wa Jall) ndiye anayefanya sababu kufanya kazi. Yapo mambo mengine yamekadiriwa kutokana na sababu zake; kunapopatikana sababu zake, basi hupatikana matunda yake. Du´aa ni moja katika sababu hizo.

[1]Muslim (1015).

[2]at-Tirmidhiy (3604) aliyesema kuwa Hadiyth ni ngeni. Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniykatika ”Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy” (3604) pasi na sentesi isemayo ”au akasamehewa madhambi yake kwa kiasi cha kile alichoomba”.

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 220-222
  • Imechapishwa: 20/04/2025