20 – Wahdat-ul-Wujuud ya Qutwub ya nyuma inafuta maneno yake ya kabla

Ni jambo linalosikitisha sana kwa mtu anayejinasibisha na Salafiyyah kuwatetea Ahl-ul-Bid´ah kwa njia kama hii ya ajabu. Hafanyi hivo kwa uadilifu wala mfumo sahihi wa ukosoaji. Hatilii nguvu ukosoaji wake dhidi ya nukuu zinazohusiana na kichwa cha khabari. Uhakika wa mambo ni kwamba wala hataji nukuu hizo, jambo ambalo ni kuwafungulia njia Ahl-ul-Bid´ah.

Kuhusiana na maneno yako ya kwamba maneno ya Qutwub katika tafsiri ya “al-Hadiyd” na “al-Ikhlaasw” hayako wazi na kwamba hayakabiliwi na maneno yake ya wazi na ya kukata kabisa yaliyoko katika “al-Baqarah”, nimeshawaraddi waliyokutangulia ´Abdullaah ´Azzaam, al-Khaalidiy na al-Qahtwaaniy kuhusiana na hilo katika “al-Aadhwaa´”.

Napenda vilevile kukujuza kuwa maneno yake katika “al-Hadiyd” na “al-Ikhlaasw” yako wazi kabisa juu ya nadharia ya kwamba viumbe wote ni Allaah na ya kwamba Allaah amekita na amechanganyika katika kila kitu. Maneno yake haya yanafuta maneno yake katika “al-Baqarah” ambapo ameraddi nadharia hii kwa ushirikiano wa Uislamu. Alifanya hilo kwa khiyari yake na kwa kalamu yake. Haya yalijulikana kwa watu kwa miaka mingi kabla ya watu kujua maneno yake katika tafsiri “al-Baqarah”. Pindi wafuasi wa Sayyid Qutwub walipoligundua hilo, wakadai kuwa aliyaandika hayo katika ile chapa ya pili ambapo yanafuta ile chapa ya kwanza na yale yaliyomo katika “al-Hadiyd” na “al-Ikhlaasw”. Kama tulivyosema tumeyaraddi katika “al-Adhwaa´” pamoja na yale ambayo punde tumeandika.