Miongoni mwa mambo yanayomkamilishia mja unyenyekevu wake kwa Allaah (´Azza wa Jall) katika Rukuu´ na Sujuud yake, ni kwamba anamsifu Mola wake kwa ushindi, ukubwa, utukufu na ujuu pale anapofanya mambo hayo. Ni kana kwamba anasema utwevu na unyenyekevu ni sifa zake ilihali ujuu, utukufu na ukubwa ni sifa Zake. Kwa ajili hiyo mja amewekewa Shari´ah katika Rukuu´ yake kusema:

سبحان ربي العظيم

“Ametakasika Mola wangu aliyetukuka, kutokamana na mapungufu yote.”

na kwenye Sujuud kusema:

سبحان ربي الأعلى

“Ametakasika  Mola wangu, Aliye juu kabisa, kutokamana na mapungufu yote.”[1]

Wakati mwingine Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akisema katika Sujuud yake:

سُبْحَانَ ذِي الجبروتِ وَالملكوتِ والْكِبْرِياءِ والْعَظَمة

“Ametakasika kutokamana na mapungufu Mwenye utawala, ufalme, ukubwa na utukufu.”[2]

Imepokewa kwamba usiku mmoja alisema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) katika Sujuud yake:

“Ninasema kama alivosema ndugu yangu Daawuud (‘alayhis-Salaam): “Namuwekea Bwana Wangu uso wangu kwenye udongo. Kwa haki kabisa nyuso zinapaswa kuwekwa  kwenye udongo.”[3]

“al-Hasan (Rahimahu Allaah) amesema:

”Unaposimama kuswali, basi simama hali ya kunyenyekea kama alivyokuamrisha Allaah. Jihadhari na kusahau na kugeukageuka. Tahadhari kwamba Allaah anakutazama na wewe unamtazama mwengine, na kwamba unamwomba Allaah Pepo na unajilinda Kwake kutokana na Moto na hali ya kuwa moyo wako haupo na hujui kile kinachosemwa na ulimi wako.”[4]

Ameipokea Muhammad bin Naswr al-Marwaziy (Rahimahu Allaah).

Amesimulia vilevile kutoka kwa ´Uthmaan bin Abiy Dahrash, ambaye ameeleza kuwa amefikiwa na khabari kwamba:

“Kuna swalah moja ambayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alisoma kwa sauti ya juu. Alipomaliza kuswali akasema: ”Je, kuna chochote kimeondoshwa kutoka katika Suurah hii?” Wakasema: ”Hatujui.” Ubayy bin Ka’b (Radhiya Allaahu ‘anh) akasema: “Ndio, Aayah fulani na fulani.” Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema: “Wana nini watu ambao wanasomewa Kitabu cha Allaah na wanashindwa kujua kile walichosomewa kutokana na kile kilichoachwa? Namna hii ndio uliondoka utukufu wa Allaah kutoka kwenye nyoyo za wana wa israaiyl; miili yao ikawepo lakini mioyo yao ikiwa haipo. Allaah hakubali kitendo chochote cha mja mpaka moyo wake uwe pamoja na mwili wake.”[5]

Kuna masimulizi mengi sana yenye maana kama hiyo.

[1] Muslim (772).

[2] Ahmad (6/24) na Abu Daawuud (859).

[3] Si Swahiyh kwa mujibu wa bn-ul-Jawziy katika “al-´Ilal al-Mutanaahiyah” (2/558).

[4] Ta´dhwiym Qadr-is-Swalaah (140).

[5] Ta´dhwiym Qadr-is-Swalaah (157).

  • Muhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn ´Abdur-Rahmaan bin Rajab al-Hanbaliy (afk. 795)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Khushuu´ fiys-Swalaah, uk. 78-81
  • Imechapishwa: 24/11/2025