Mtu anahitaji kutimiza sharti mbili ili awe mlinganizi:

1 – Ni lazima alinganie kwa Allaah (´Azza wa Jall) kwa kumtakasia Yeye nia.

2 – Ni lazima alinganie kwa elimu na utambuzi. Mjinga haifai kulingania kwa sababu ataharibu zaidi kuliko atakavyotengeneza. Pengine akahalalisha haramu na akaharamisha halali. Pengine akajibu kwa ujinga. Pengine akajibu kimakosa. Mlinganizi anakutana na mambo yenye kumtatiza, vipingamizi na watu wanaowababaisha watu. Kwa ajili hiyo ni lazima awe na elimu ili kuzizuia hoja zao tata na upotofu wao. Asiyekuwa na elimu hawezi kuzisambaratisha hoja tata za walaghai na matapeli. Hawezi jambo hilo isipokuwa yule ambaye yuko na elimu na utambuzi. Allaah (Ta´ala) amesema:

أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي

“… mimi na anayenifuata.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wafuasi wake wanaolingania kwa utambuzi wanalingania kwa Allaah. Wanalingania kwa Allaah na si kwa mwengine asiyekuwa Allaah, na wanalingania kwa utambuzi na si kwa ujinga. Watu hawa ndio wafuasi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtu hawi mlinganizi anayemfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) isipokuwa aliyesifika kwa sifa hizi. Anayekosa moja kati yazo hawi juu ya njia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

وَسُبْحَانَ اللَّـهِ

”… na Utakasifu ni wa Allaah… ”

Bi maana kumtakasa Allaah kutokana na yale yasiyolingana Naye:

وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ

”… nami si miongoni mwa washirikina.”[1]

Najitenga mbali nao na kutokana na dini yao. Yule asiyejitenga mbali kutokana na shirki na washirikina halinganii kwa Allaah.

[1] 12:108

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 47
  • Imechapishwa: 29/07/2024