Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab amesema:

Ya wajibu ni mambo nane:

1- Takbiyr zote mbali na Takbiyrat-ul-Ihraam.

2- Kusema:

سبحان ربي العظيم

“Subhaana Rabbiy ´al-´Adhwiym”

katika Rukuu´.

3-  Kusema:

سَمِعَ اللهُ لِمَنْ حَمِدَه

“Sami´ Allaahu li man hamidah”

kwa imamu na kwa anayeswali peke yake.

4- Kusema:

رَبَّنَا وَ لَكَ الْحَمْدُ

“Rabbanaa wa lak al-Hamd”

Itasemwa na wote.

5- Kusema:

سبحان ربي الأعلى

“Subhaana Rabbiy al-A´laa”

katika Sujuud.

6- Kusema:

رَبِّ اغْفِرْ لِي

“Rabb Ighfir liy”

baina ya Sajdah mbili.

7- Tashahhud  ya kwanza.

8- Kukaa katika Tashahhud hiyo.

MAELEZO

Baada ya Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab bin Sulaymaan bin Haadiy at-Tamiymiy (Rahimahu Allaah), Shaykh-ul-Islaam na mujadidi katika kisiwa cha kiarabu wakati wake, kutaja masharti na nguzo za swalah, ndipo akataja mambo nane ya wajibu ya swalah. Kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanachuoni mambo ya wajibu ya swalah ni nane:

1- Takbiyr zote mbali na Takbiyrat-ul-Ihraam. Kuhusu Takbiyrat-ul-Ihraam ni nguzo ambayo ni lazima kuitekeleza. Swalah haisihi isipokuwa kwayo, ni mamoja kwa kukusudia au kwa kusahau. Swalah haisihi pasi na Takbiyrat-ul-Ihraam. Ni lazima ipatikane.

Imeitwa Takbiyrat-ul-Ihraam kutokana na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

 ”Ufunguo wa swalah ni twahara. Uharamu [ufunguzi] wake ni Takbiyr na uhalali [ufungwaji] wake ni Tasliym.”

Takbiyr hii ni ya wajibu kwa mtazamo wa wanachuoni wote Inasemwa namna hii:

الله أكبر

“Allaah ni mkubwa.”

Haya ndio maoni ya wanachuoni wengi. Si sahihi kusema kitu kingine zaidi ya:

الله أكبر

“Allaah ni mkubwa.”

Si sahihi kusema “Allaah ni mtukufu” au “Allaah ndiye msikivu zaidi”. Ni lazima iwe kwa tamko:

الله أكبر

“Allaah ni mkubwa.”

Hivo ndivo ilivyotajwa katika maandiko. Maana yake ni kwamba Allaah ndiye mkubwa kuliko kila kikubwa na ndiye mtukufu kuliko kila kitukufu.

Kuhusu Takbiyr wakati wa kurukuu, kusujudu, kuinuka kutoka kwenye Rukuu´ na Takbiyr zengine zote ni wajibu kwa mujibu wa baadhi ya wanachuoni. Ndio maoni sahihi. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alizihifadhi na akasema:

“Swalini kama mlivyoniona nikiswali.”

 Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliposahau Tashahhud ya kwanza aliilipiza kwa kuleta sujudu ya kusahau. Ni dalili inayoonyesha kwamba kitendo hicho ni wajibu. Wanachuoni wengi wanaonelea kuwa imependekezwa tu. Swalah haibatiliki ikiwa itaachwa, si kwa kukusudia wala kwa kusahau. Maoni yaliyo karibu zaidi na usawa ni kwamba ni wajibu midhali mtu atakumbuka, lakini ikiachwa kwa sababu ya kusahau au kwa sababu ya ujinga, hakuna neno. Kwa hiyo swalah ni sahihi ikiwa mtu atasahau au akaacha kwa sababu ya ujinga kusema:

الله أكبر

“Allaah ni mkubwa.”

wakati kurukuu au:

سَمِعَ اللهُ لِمَنْ حَمِدَه

“Sami´ Allaahu li man hamidah”

wakati wa kuinuka kutoka kwenye Rukuu´. Hata hivyo haijuzu kwa mtu kukusudia kuiacha. Mtu akiacha kusema hivo kwa sababu ya kusahau anatakiwa kusujudu Sujuud mbili za kusahau.

2- Kusema:

سبحان ربي العظيم

“Subhaana Rabbiy ´al-´Adhwiym”

katika Rukuu´.

3-  Kusema:

سَمِعَ اللهُ لِمَنْ حَمِدَه

“Sami´ Allaahu li man hamidah”

kwa imamu na kwa anayeswali peke yake.

4- Kusema:

رَبَّنَا وَ لَكَ الْحَمْدُ

“Rabbanaa wa lak al-Hamd”

Itasemwa na wote.

5- Kusema:

سبحان ربي الأعلى

“Subhaana Rabbiy al-A´laa”

katika Sujuud.

6- Kusema:

رَبِّ اغْفِرْ لِي

“Rabb Ighfir liy”

baina ya Sajdah mbili.

7- Tashahhud  ya kwanza.

8- Kukaa katika Tashahhud hiyo.

Zote hizi nane ni wajibu kwa mtu azifanye pale ambapo mtu atakumbuka na akawa anajua, zinaanguka ikiwa mtu atakuwa hajui au akasahau. Ikiwa imamu au ambaye anaswali peke yake ataacha moja wapo, basi anatakiwa kusujudu Sujuud mbili kwa sababu ya kusahau. Ama kuhusu yule anayeswalishwa anamfuata imamu wake. Lakini imamu na yule anayeswali peke yake wanatakiwa kuilipiza kwa kusujudu Sujuud mbili kwa sababu ya kusahau. Dalili ya hilo ni maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Swalini kama mlivyoniona nikiswali.”

Jengine Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisujudu Sujuud mbili za kusahau wakati aliposahau kuleta Tashahhud ya kwanza. Sujuud mbili hizi za kusahau alizileta kabla ya Tasliym.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ash-Sharh al-Mumtaaz, uk. 126-130
  • Imechapishwa: 15/07/2018