Kitenguzi cha kwanza ndio cha khatari zaidi na kibaya zaidi. Nacho si kingine ni kushirikisha katika ´ibaadah ya Allaah (´Azza wa Jall).

´Ibaadah – Limechukuliwa kutoka katika kuabudu, kudhalilika na kunyenyekea kwa khiyari. Vilevile kujikurubisha kwa Allaah kwa yale aliyoyawekea Shari´ah. Hii ndio ´ibaadah.

Baadhi ya wanachuoni wanaiarifisha kwa kusema ni mapenzi na udhalilikaji wa hali ya mwisho. Mapenzi ya hali ya mwisho kwa Allaah (´Azza wa Jalla) pamoja na kujidhalilisha Kwake[1]. Hii ndio maana yake ya kijumla.

Kuhusu maana yake kwa upambanuzi ni kama alivyosema Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah):

“Ibaadah ni neno lililokusanya kila kile anachokipenda Allaah na kukiridhia katika matendo na maneno, ya dhahiri na yaliyojificha.”[2]

Hii ndio maana ya ´ibaadah kwa maana yake yenye kuenea. Ni neno lililokusanya kila kile anachokipenda Allaah na kukiridhia katika matendo na maneno, ya dhahiri na yaliyojificha. Kuna ´ibaadah ambazo zinakuwa waziwazi mdomoni na kupitia viungo vya mwili. Kuna ´ibaadah zengine zinakuwa zimejicha ndani ya moyo. Aina zake ni nyingi. Zimetajwa katika Qur-aan na Sunnah.

Pale tuliposema kwamba ´ibaadah ni kule kudhalilika na kunyenyekea kwa kutaka kwa mtu mwenyewe kunavuliwa katika hayo kule kudhalilika na kunyenyekea kwa kutenzwa nguvu. Kila mtu ni mja wa Allaah. Ni mamoja awe muumini au awe kafiri. Kwa maana kwamba ni wenye kunyenyekea na ni wenye kujisalimisha juu ya makadirio ya Allaah (Jalla wa ´Alaa) yenye kupitika kwao. Wao ni waja wa Allaah ambao anawaendesha vile anavotaka. Hakuna yeyote anayetoka katika mipango na makadirio Yake. Amesema (Ta´ala):

إِن كُلُّ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ إِلَّا آتِي الرَّحْمَـٰنِ عَبْدًا

“Hakuna yeyote yule aliyeko katika mbingu na ardhi isipokuwa atamjia ar-Rahmaan, akiwa ni mja.” (Maryam 19:93)

Huu ndio uja wenye kuenea. Sio wa khiyari. Bali ni wa utenzwaji nguvu. Amesema (Ta´ala):

وَلَهُ أَسْلَمَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ طَوْعًا وَكَرْهًا وَإِلَيْهِ يُرْجَعُونَ

“… na hali amejisalimisha Kwake kila aliye katika mbingu na katika ardhi – kwa kupenda [au] kwa kutokupenda – na Kwake watarejeshwa.” (Aal ´Imraan 03:83)

Pale tuliposema:

“Kujikurubisha Kwake kwa yale aliyoyawekea Shari´ah.”

Kunavuliwa katika hayo kujikurubisha Kwake kwa yale ambayo hakuyawekea Shari´ah katika Bid´ah na mambo yaliyozuliwa. Ni lazima kujikurubisha kwa Allaah kuwe kwa yale aliyoyawekea Shari´ah kwa waja wake na kupitia Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ama mtu kujizushia ´ibaadah yako mwenyewe, kutoka kwa Shaykh wako au kutoka kwa fulani na fulani mbali na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi hiyo itakuwa ni ´ibaadah iliyozuliwa na ya batili yenye kurudishwa. Kama alivyosema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule atakayefanya matendo yasiyoafikiana na amri yetu, basi itarudishwa mwenyewe.”[3]

“Yule atakayezua katika amri yetu hii yale yasiyokuwemo, atarudishiwa mwenyewe.”[4]

Na akasema(Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Tahadharini na mambo yaliyozuliwa! Kwani hakika kila kitachozuliwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu na kila upotevu ni Motoni.”[5]

Hii ndio maana ya ´ibaadah.

[1] Tazama “Majmuu´-ul-Fataawa” (10/153).

[2] Tazama “Majmuu´-ul-Fataawa” (10/149).

[3] Ameipokea Muslim (18/1718) kupitia kwa ´Aishah (Radhiya Allaahu ´anhaa).

[4] Ameipokea al-Bukhaariy (2697) na Muslim (1718) kupitia kwa ´Aishah (Radhiya Allaahu ´anhaa).

[5] Ameipokea Abu Daawuud (4607), at-Tirmidhiy (2676) na Ibn Maajah (42). at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 40-41
  • Imechapishwa: 04/07/2018