20. Kuamini Uonekanaji siku ya Qiyaamah

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Inatakiwa kuamini kuonekana kwa Allaah siku ya Qiyaamah. Kumepokelewa Hadiyth nyingi Swahiyh kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusiana na suala hili.”

MAELEZO

Kuna dalili nyingi juu ya kumuona Allaah (´Azza wa Jall) huko Aakhirah. Miongoni mwa dalili hizo ni maneno ya Allaah (Ta´ala):

لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ

“Kwa wale waliofanya wema watapata mazuri kabisa na ziada.”[1]

Ziada imefasiriwa kwamba ni waumini kumuona Allaah siku ya Qiyaamah, kama ilivyokuja katika Hadiyth ya Swuhayb (Radhiya Allaahu ´anh)[2]. Nyingine ni maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاضِرَةٌ إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ

“Nyuso siku hiyo zitang´ara – zikimtazama Mola wake.”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema katika Hadiyth Swahiyh:

“Hakika nyinyi mtamuona Mola wenu kama mnavyouona mwezi huu mwandamo – hamtosongamana katika kumuona.”[4]

Kuna Hadiyth zengine nyingi zilizopokelewa juu ya maudhui haya. Zinaweza hata kufikia kiwango cha kupokelewa kwa njia nyingi kimaana. Zote zinafidisha kwamba waumini watamuona Mola wao siku ya Qiyaamah kama wanavyouona mwezi usiku mwandamo pasi na mawingu na kama wanavyoona jua waziwazi pasi na mawingu. Hapa kuna kufananisha kati  ya kuona na kuona na si kufananisha kati ya vyenye kuonekana. Jua na mwezi ni viumbe vilivoumbwa na Allaah. Mfano huo umepigwa ili kuonekana kunakokusudiwa kufahamike. Kama ambavyo mwezi na jua siku isiyokuwa na mawingu vinaonekana bila mtu kuvizunguka, hivyo ndivo Allaah ataonekana huko Aakhirah pasi na kuzungukwa.

[1] 10:26

[2] at-Tirmidhiy (2552). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwilaal-ul-Jannah” (472).

[3] 75:22-23

[4] al-Bukhaariy (554) na Muslim (633).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 104-106
  • Imechapishwa: 22/04/2019