20. Hivi ndivo wanavoamini Ahl-ul-Hadiyth, Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah

98 – Imaam Abu Bakr al-Ismaa´iyliy (Rahimahu Allaah) amesema:

”Tambua – Allaah aturehemu sisi na nyinyi – ya kwamba madhehebu ya Ahlul-Hadiyth, Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah yamejengwa juu ya kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake na kuyakubali yaliyosemwa na Qur-aan na mapokezi yaliyosihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hayatakiwi kurudishwa na wala hakuna namna ya kufanya hivo. Haya ni kwa sababu wameamrishwa kufuata Qur-aan na Sunnah. Wanaona kuwa humo mna dhamana ya uongofu na wanashuhudia ya kwamba Mtume wao (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anaongoza katika Njia iliyonyooka na wakati huo huo wanatahadhari juu ya fitina na adhabu iumizayo kwa kwenda kinyume na viwili hivyo.

Wanaitakidi kuwa Allaah anaombwa kwa majina Yake Aliyojiita nayo Mwenyewe, sifa Zake Alizojisifia nazo Mwenyewe na yale majina na sifa aliyomwita na kumsifia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Amemuumba Aadam kwa mikono Yake. Mikono Yake ni yenye kukunjuliwa na anatunuku Atakavyo.

Hili halitakiwi kufanyiwa namna. Kadhalika (´Azza wa Jall) amelingana juu ya ´Arshi. Hili pia halitakiwi kufanyiwa namna, kwa sababu Allaah (Ta´ala) amelingana juu ya ´Arshi pasi na kuelezea namna alivyolingana.”[1]

al-Ismaa´iyliy alikuwa ni miongoni mwa maimamu wakubwa. Alikusanya Fiqh na Hadiyth, akatunga ”as-Swahiyh” na wanazuoni wakasoma kwake Jurjaan. Alifariki mwaka wa 371 akiwa na 94. ad-Daaraqutwniy amesema pamoja na utukufu wake:

”Niliazimia zaidi ya mara moja kusafiri kwenda kwa Abu Bakr, lakini sikujaaliwa.”

Kijitabu chake hichi cha  ´Aqiydah tumekisikia kikisimuliwa kutoka kwake kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

[1] I´tiqaadu A’immati Ahl-il-Hadiyth, uk. 396

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy (afk. 748)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Arba´iyn fiy Swifaati Rabb-il-´Aalamiyn, uk. 94-95
  • Imechapishwa: 05/06/2024