2. Matahadharisho juu ya Bid´ah na watu wake

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“… kuepukana na Bid´ah kwani kila Bid´ah ni upotevu… “

MAELEZO

Ni wajibu kujitenga mbali na Bid´ah za wenye kupotosha kwa sababu wanapiga vita Sunnah. Kadhalika ni wajibu kuifahamu misingi ya ´Aqiydah na kushikamana barabara na Qur-aan na Sunnah na kuifahamu sahihi kama walivyofahamu Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Baadaye wakapokea watu wa karne bora katika maimamu wa elimu na wakawanukulia wale waliokuja baada yao. Wakakomeka na Sunnah na hawakuzusha chochote katika dini ya Allaah. Hawakuzusha ´ibaadah yoyote mpya. Ahl-ul-Bid´ah ndio wenye kuzusha kwa sababu ya uchache wa elimu yao yenye manufaa na ufahamu wa sahihi. Hayo ni kutokana na madhambi yao, kuitanguliza kwao akili mbele kabla ya Qur-aan na Sunnah. Yule mwenye kutanguliza mbele akili kabla ya Qur-aan na Sunnah anapotea. Qur-aan na Sunnah ndivyo vinaihukumu akili. Wale waliopotea  na wakazusha wametoka na kuiacha njia ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na hawakushikamana na misingi yao. Matokeo yake wakawa ni Ahl-ul-Bid´ah.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitahadharisha maneno na matendo ya kizushi, ni mamoja zenye kuonekana na zenye kufichikana. al-´Irbaadh bin Saariyah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nakutahadharisheni na mambo yaliyozuliwa, kwani hakika kila kilichozuliwa ni Bi´dah.”[1]

Watunzi wa Sunan wameongeza:

“Nakutahadharisheni na mambo yaliyozuliwa, kwani hakika kila kilichozuliwa ni Bi´dah na kila upotofu ni Motoni.”[2]

Anafanya hivi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa ajili ya kuwafanya watu waogope kutokamana na Bid´ah. Bid´ah zina khatari. Mwenye kuzusha amezidisha katika Uislamu. Uislamu umekamilika kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah. Allaah (´Azza wa Jall) ametubainishia pale aliposema:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

 “Leo wamekata tamaa wale waliokufuru juu ya dini yenu, hivyo basi msiwaogope na niogopeni Mimi. Leo nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni Uislamu uwe dini yenu.”[3]

Kuhusu Sunnah imethibiti kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule atakayezusha katika amri yetu hii kisichokuwemo atarudishiwa mwenyewe.”[4]

Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumwacha ndege anayepiga kwa mbawa zake mbinguni isipokuwa ametufunza kitu juu yake.”[5]

Kwa msemo mwingine ni kwamba watu wameamrishwa kufuata na wamekatazwa kuzusha. Hawana chaguo jengine isipokuwa kufuata Qur-aan na Sunnah kwa ufahamu na mfumo wa Salaf. Haijuzu kuiacha njia hii na kwenda kwa Ahl-ul-Bid´ah waliopotea na watu wenye fikira zinazokinzana na ´Aqiydah sahihi ya Kiislamu na njia yake iliyosalimina na kunyooka.

[1] Muslim (867).

[2] an-Nasaa’iy (1578).

[3] 05:03

[4] al-Bukhaariy (2697).

[5] Muslim (1718).

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 19-20
  • Imechapishwa: 30/09/2019