Msingi wa unyenyekevu ni ulaini wa moyo, upole, utulivu, unyenyekevu, kuzivunjavunja na uchungu. Moyo unaponyenyekea, basi sehemu zingine za mwili na viungo hufuata na kunyenyekea, kwa sababu hufuata moyo. Kama alivyosema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):

“Zindukeni! Hakika kwenye mwili kuna kipande cha nyama; kinapotengemaa basi hutengemaa mwili mzima, na kinapoharibika basi huharibika mwili mzima. Nacho ni moyo.”[1]

Pindi moyo unaponyenyekea basi usikizi, uoni, kichwa, uso na viungo vingine vyote na kila kitu kinachotokana navyo vinanyenyekea mpaka maneno. Kwa ajili hiyo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akisema:

خَشَعَ لَكَ سَمْعِي، وَبَصَرِي، وَمُخِّي، وَعَظْمِي، وَعَصَبِي

“Kwako nimejisalimisha, umenyenyekea Kwako usikizi wangu, uoni wangu, ubongo wangu, mfupa wangu na hisia zangu.”[2]

Imekuja katika upokezi mwingine:

وما استقلَّت به قدمي

”… na ambacho kimesimama juu ya miguu yangu.”[3]

Katika Salaf wako walimuona mswaliji anayecheza na mkono wake ndani ya swalah wakasema:

”Lau ungenyenyekea moyo wa huyu basi vingenyenyekea viungo vyake.”

Hayo yamepokelewa pia kutoka kwa Hudhayfah (Radhiya Allaahu ´anh) na Sa’iyd bin al-Musayyab. Vilevile yamepokewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwa cheni isiyokuwa Swahiyh.

al-Mas´uudiy amesimulia kutoka kwa Abu Sinaan, ambaye amesimulia kutoka kwa mtu, ambaye amesimulia kutoka kwa ‘Aliy bin Abiy Twaaalib (Radhiya Allaahu ´anh), ambaye amesema kuhusu maneno Yake (Ta’ala):

قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ

“Hakika wamefaulu waumini; ambao katika swalah zao ni wenye kunyenyekea.”[4]

”Ni kule kuwa na unyenyekevu moyoni, kuwa mlaini mbele ya muislamu na usijigeuzegeuze ndani ya swalah yako.”[5]

´Atwaa’ bin as-Saa-ib amesimulia kutoka kwa bwana mmoja, ambaye ameeleza kuwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh), ambaye amesema:

”Unyenyekevu ni unyenyekevu wa moyo na usijigeuze kuliani wala kushotoni.”

´Aliy bin Abiy Twalhah amesimulia kwamba Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema kuhusiana na maneno Yake (Ta´ala):

قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ

“Hakika wamefaulu waumini; ambao katika swalah zao ni wenye kunyenyekea.”

”Kwa maana ni wenye khofu na watulivu.”

Ibn Shawdhab amesimulia kwamba al-Hasan (Rahimahu Allaah) amesema:

”Unyenyekevu ulikuwa kwenye nyoyo zao ambapo wakainamisha macho yao wakati wanaswali.”

Ibn Abiy Najiyh amesimulia kwamba Mujaahid (Rahimahu Allaah) amesema kuhusiana na maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّهُمْ كَانُوا يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَيَدْعُونَنَا رَغَبًا وَرَهَبًا ۖ وَكَانُوا لَنَا خَاشِعِينَ

“Hakika wao walikuwa wakikimbilia katika mambo ya kheri na wakituomba kwa matumaini na khofu na walikuwa Kwetu wenye kunyenyekea.”[6]

”Kwa maana wanyenyekevu.”

[1] al-Bukhaariy (52) na Muslim (1599).

[2] Muslim (771).

[3] Ahmad (960).

[4] 23:01-02

[5] al-Haakim (3/393), ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[6] 21:90

  • Muhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn ´Abdur-Rahmaan bin Rajab al-Hanbaliy (afk. 795)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Khushuu´ fiys-Swalaah, uk. 29-35
  • Imechapishwa: 24/11/2025