193. Mambo ya wajibu yote ya Uislamu ni yenye kutekelezeka

Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

146 – Allaah (Ta´ala) hakuwalazimisha kufanya isipokuwa yale wanayoyaweza, na wala hawawezi kufanya isipokuwa yale aliyowalazimisha.

MAELEZO

Allaah (Ta´ala) amesema:

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

“Allaah hakalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kadiri ya uwezo wake.”[1]

يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ

“Allaah anakutakieni mepesi na wala hakutakieni magumu.”[2]

Allaah hawalazimishi waja isipokuwa yale wanayoweza kufanya, isipokuwa kama ni kwa ajili ya kutaka kuwaadhibu. Kama ambavo Allaah aliwawajibishia wana wa israaiyl mambo mengine magumu kwa sababu ya kuchupa kwao mpaka:

فَبِظُلْمٍ مِّنَ الَّذِينَ هَادُوا حَرَّمْنَا عَلَيْهِمْ طَيِّبَاتٍ أُحِلَّتْ لَهُمْ وَبِصَدِّهِمْ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ كَثِيرًاوَأَخْذِهِمُ الرِّبَا وَقَدْ نُهُوا عَنْهُ وَأَكْلِهِمْ أَمْوَالَ النَّاسِ بِالْبَاطِلِ ۚ وَأَعْتَدْنَا لِلْكَافِرِينَ مِنْهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا

“Basi kwa dhuluma ya mayahudi, Tuliwaharamishia vilivyo vizuri walivyohalalishiwa na kwa sababu ya kuwazuilia kwao wengi kutokana na Njia ya Allaah, na kuchukua kwao ribaa na hali wamekatazwa na kula kwao mali za watu kwa batili, na tumewaandalia makafiri katika wao adhabu iumizayo.”[3]

Matokeo yake Allaah akawaadhibu kwa kuwawajibishia mambo ambayo hawayawezi. Kwa ajili hiyo imekuja katika du´aa:

رَبَّنَا وَلَا تَحْمِلْ عَلَيْنَا إِصْرًا كَمَا حَمَلْتَهُ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِنَا

“Mola wetu! Usitubebeshe mzigo kama ulivyowabebesha wale waliokuwa kabla yetu.”[4]

Allaah, kutokana na fadhilah, ihsani na rehema Yake, hawawajibishii waja isipokuwa yale mambo wayawezayo. Yeye ni Mwenye kurehemu:

إِنَّ اللَّـهَ بِالنَّاسِ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Hakika Allaah kwa watu ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.”[5]

Hata hivyo ni jambo linatakiwa kuangaliwa vyema kusema kwamba hawawezi zaidi ya vile alivyowawajibishia. Bali wanaweza zaidi ya yale aliyowawajibishia, lakini Allaah anawatakia mepesi na hawatakii magumu. Allaah amewaondoshea waja magumu, amewawekea katika Shari´ah dini nyepesi na amewakataza kuzidisha ile mipaka ya kati na kati. Haijuzu kwa mtu kukesha usiku mzima anaswali na wala haijuzu kwake kuacha kuoa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Lakini mimi nalala na naswali, nafunga na nafungua, naoa na nala nyama. Yeyote atakayezipa mgongo Sunnah  zangu basi si katika mimi.”[6]

Allaah hawawajibishi yale yatakayowatia uzito. Angelifanya hivo, basi wangeliweza. Hata hivyo Allaah haridhii juu yao mambo magumu na mazito.

[1]2:286

[2]2:185

[3]4:160-161

[4]2:286

[5] 2:143

[6]al-Bukhaariy (5063) na Muslim (1401).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 212-213
  • Imechapishwa: 14/04/2025