Ibn Taymiyyah amesema:

Alimwamrisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aseme:

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي

“Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah, juu ya ujuzi na umaizi – mimi na anayenifuata.”[1]

Allaah amemwamrisha Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) awafikishie watu wote kwamba ”hii ndio njia yangu”. Bi maana njia yangu ninayopita. Ni ipi njia hiyo? Njia ambayo analingania kwa Allaah kwa utambuzi na umaizi. Njia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambayo ametumwa kwayo ni kwamba analingania kwa Allaah, halinganii kwa nafsi yake. Ulinganizi wake haukuwa umejengeka katika mapato ya kidunia, uongozi au utawala. Analingania kwa Allaah. Hii ni moja katika zile sharti za kulingania kwa Allaah ya kwamba iwe kwa ajili ya Allaah pekee, na mtu asikusudie kujionyesha, kutaka kusikika wala ukubwa. Lengo la mlinganizi iwe kuwanufaisha watu na kuwaondoa kutoka katika viza na kuingia ndani ya nuru. Huu ndio ulinganizi kwa Allaah. Kuhusu anayelingania ili aadhimishwe, atukuzwe, aheshimiwe, apewe mali au aongeze, au analingania katika vyamavyama au katika kundi au madhehebu yasiyokuwa ya Ahl-us-Sunnah halinganii kwa Allaah; analingania kwa mwengine. Kwa hivyo sio kila anayelingania analingania kwa Allaah. Isipokuwa tu yule ambaye malengo yake ni kuwafanya watu waweze kumtambua Allaah, warejee kwa Allaah, kuwafunza watu haki, kuwaonya kutokana na upotofu, shirki na Bid´ah ndiye ambaye analingania kwa Allaah (´Azza wa Jall) kikweli. Kuna walinganizi wengi, lakini wanaolingania kwa Allaah ni wachache. Allaah pekee ndiye anayejua ni kipi wanalingania kwacho.

[1] 12:108

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 46-47
  • Imechapishwa: 29/07/2024