19. Ulazima wa kutaja jina la Allaah kabla ya kutawadha

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

Ni wajibu kusema “Bismillaah” mtu akikumbuka hilo.

MAELEZO

Hii ni mojawapo ya maoni katika masuala haya, nayo ni riwaya kutoka kwa Imaam Ahmad. Miongoni mwa waliosema hivo ni al-Hasan na Ishaaq.

Maoni ya pili ni kwamba kutaja jina la Allaah ni jambo linalopendeza, nayo ndio maoni ya jopo kubwa la wanazuoni na ni mojawapo ya riwaya mbili kutoka kwa Imaam Ahmad. Hayo yametajwa katika ”al-Mughniy” (1/145). Imepokelewa kuhusu kutaja jina la Allaah katika wudhuu´ Hadiyth isemayo:

“Hana wudhuu´ asiyetaja jina la Allaah juu yake.”

Ameipokea Abu Daawud (101) na wengine kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh). Shaykh al-Albaaniy amesema kuwa ni Hadiyth nzuri na akasema:

“Imetiwa nguvu na Haafidhw al-Mundhiriy na al-´Asqalaaniy, ilihali Hasan na Ibn-us-Swalaah, Ibn Kathiyr na al-´Iraaqiy wameonelea kuwa ni nzuri.” Tazama ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (81).

Uchaguzi wa Shaykh wa kusema kuwa kutaja jina la Allaah ni waajibu ikiwa mtu atakumbuka kunaonyesha kushika tahadhari na kutoka nje ya tofauti. Mfano wa hili ni yale aliyoyasema (Rahimahu Allaah) katika ”Adab-ul-Mashiy ilaas-Swalaah”:

“Takbiyrat-ul-Ihraam inatosheleza badala ya Takbiyr ya kurukuu, kutokana na kitendo cha Zayd bin Thaabit na Ibn ´Umar. Haijulikani kwamba kuna Swahabah yoyote ambaye aliona kinyume na wao. Lakini kuleta zote mbili ndio bora zaidi ili kutoka kwenye tofauti ya waliolazimisha kuleta zote mbili.”

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-Muhsin bin Hamad al-´Abbaad
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 20-21
  • Imechapishwa: 25/05/2026