19. Subiri, karibuni dunia inafika mwisho!

Basi alipojaribiwa mja na kile alichojaribiwa nacho, akasaidiwa kwa majeshi na zana na ngome na akaambiwa apambane na adui yako na ampige vita. Basi haya ni majeshi na chukua utakavyo. Hizi ni ngome, basi jikinge katika ngome yoyote utakayo miongoni mwa hizi na kaa kwenye mpaka hadi kufa. Hakika jambo hili ni karibu na muda wa kulinda ni mfupi sana. Basi ni kama kwamba mfalme mkuu amekwishakukutumia wajumbe wake wakakuhamisha kwenda katika nyumba yake, ukapumzika kutokana na vita hivyo na akakutenganisha na adui yako na ukaachiliwa huru katika nyumba yake ya heshima ambapo ukibadilika ndani yake utakavyo na adui yako akafungwa katika jela kali zaidi na unamwona. Kwa hiyo gereza ambalo alikuwa anataka kukuingiza humo, sasa yeye ndilo ameingizwa humo, milango imefungwa juu yake na akakata tamaa na rehema na faraja. Wewe upo katika yale yaliyo matamanio ya nafsi yako na utulivu wa jicho lako. Hayo ni malipo ya subira yako katika kipindi hicho kifupi na ulindaji wako wa mpaka kwa ajili ya Mola wako. Haikuwa isipokuwa ni saa moja tu kisha ikaisha. Ni kama kwamba ugumu haukuwahi kuwepo kabisa.

Ikiwa nafsi imedhoofika kutokana na kutafakari ufupi wa muda na uharaka wa kuisha kwake, basi aitafakari Aayah Yake (Ta´ala):

كَأَنَّهُمْ يَوْمَ يَرَوْنَ مَا يُوعَدُونَ لَمْ يَلْبَثُوا إِلَّا سَاعَةً مِّن نَّهَارٍ

”Siku watakayoona waliyoahidiwa itakuwa kama kwamba hawakubakia [ulimwenguni] isipokuwa saa moja tu katika mchana.”[1]

كَأَنَّهُمْ يَوْمَ يَرَوْنَهَا لَمْ يَلْبَثُوا إِلَّا عَشِيَّةً أَوْ ضُحَاهَا

”Siku watakapoiona watakuwa kama kwamba hawakubakia [ulimwenguni] isipokuwa jioni moja au mchana wake.”[2]

قَالَ كَمْ لَبِثْتُمْ فِي الْأَرْضِ عَدَدَ سِنِينَ قَالُوا لَبِثْنَا يَوْمًا أَوْ بَعْضَ يَوْمٍ فَاسْأَلِ الْعَادِّينَ قَالَ إِن لَّبِثْتُمْ إِلَّا قَلِيلًا ۖ لَّوْ أَنَّكُمْ كُنتُمْ تَعْلَمُونَ

”Atasema: ”Muda gani mlikaa katika ardhi kwa idadi ya miaka?” Watasema: ”Tulikaa siku au sehemu ya siku, basi waulize wanaohesabu.” Atasema: ”Hamkukaa [ulimwenguni] isipokuwa kidogo tu, laiti mngelikuwa mnajua.”[3]

يَوْمَ يُنفَخُ فِي الصُّورِ ۚ وَنَحْشُرُ الْمُجْرِمِينَ يَوْمَئِذٍ زُرْقًا يَتَخَافَتُونَ بَيْنَهُمْ إِن لَّبِثْتُمْ إِلَّا عَشْرًا نَّحْنُ أَعْلَمُ بِمَا يَقُولُونَ إِذْ يَقُولُ أَمْثَلُهُمْ طَرِيقَةً إِن لَّبِثْتُمْ إِلَّا يَوْمًا

”Siku litakapopulizwa baragumu na tutawakusanya wahalifu Siku hiyo macho yao yakiwa rangi ya kibuluu. Wakinong’onezana kati yao: ”Hamkukaa [ulimwenguni] isipokuwa [siku] kumi tu. Sisi Tunajua zaidi watakayoyasema. Atakaposema mbora wao katika mwendo: ”Hamkukaa isipokuwa siku moja tu.”[4]

Siku moja Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwakhutubia Maswahabah wake. Wakati alipokuwa juu ya jua juu ya vichwa vya milima, kwa maana wakati wa jua kuzama, akasema:

“Hakika haijabakia katika ulimwengu kutoka kilichotangulia isipokuwa kama kilichobakia katika siku yenu hii kutokana na kilichotangulia.”[5]

Basi na azingatie mtu mwenye akili na anayejinasihi Hadiyth hii na ajue ni kitu gani amekipata kutoka katika wakati huu uliosalia katika dunia nzima, ili ajue kwamba yuko katika udanganyifu na ndoto zisizo na maana na kwamba ameiuza furaha ya milele na neema ya kudumu kwa fungu duni lisilo na thamani yoyote. Lau angeliitafuta radhi ya Allaah (´Azza wa Jall) na nyumba ya Aakhirah, basi Allaah angempa hilo fungu kwa ukamilifu zaidi na kilicho bora kuliko hicho. Kama ilivyo katika baadhi ya masimulizi:

“Ewe mwana wa Aadam! Uza ulimwengu kwa ajili ya Aakhirah na hivyo utavipata vyote viwili, na wala usiuze Aakhirah kwa ajili yaulimwengu utavikosa vyote viwili.”[6]

[1] 46:35

[2] 79:46

[3] 23:112-114

[4] 20:102-104

[5] at-Tirmidhiy (2191), aliyesema kuwa Hadiyth ni nzuri na Swahiyh, Ahmad (4/51-52), Abu Ya´laa (1101) na ´Abd bin Humayd (862). Nzuri kwa mujibu wa Ibn Hajar katika “al-Amaaliy al-Mutwlaqah” (170), dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan at-Tirmidhiy” (2191).

[6] Yamesemwa na al-Hasan al-Baswriy katika “Hilyat-ul-Awliyaa” (2/143).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 33-35
  • Imechapishwa: 04/08/2025