19. Ndio ´Aqiydah yangu, ya baba yangu na ya maimamu wote

Haafidhw Abu Bakr bin Abiy Daawuud as-Sijistaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Shikamana na Kamba ya Allaah na ufuate uongofu

usiwe mzushi huenda ukafaulu

Fuata katika dini yako Kitabu cha Allaah na Sunnah ambazo

zimekuja kutoka kwa Mtume wa Allaah utafaulu na kufaidika

Sema “Hayakuumbwa maneno ya Mfalme Wetu” –

hivyo ndivyo walivyoamini wachaji Allaah na wakalidhihirisha

Usichukue msimamo wa kusita juu ya Qur-aan

kama walivyosema wafuasi wa Jahmiy na wakazembea

Wala usiseme kuwa kisomo cha Qur-aan kimeumbwa

kwani hakika maneno ya Allaah yanawekwa wazi kwa matamshi

Hakika Jahmiy atapinga pia mkono Wake wa kuume –

na mikono Yake yote miwili kwa fadhilah ni yenye kutoa

Sema anashuka kuja kwenye mbingu ya dunia ili atunuku fadhilah Zake

milango ya mbingu hufunguliwa

Wameyapokea hayo watu zisizorudishwa Hadiyth zao

Tanabahini! Wamekula khasara watu waliowakadhibisha na wabezwe[1]

Ibn Abiy Daawuud amesema:

”Hii ndio ´Aqiydah yangu, ´Aqiydah ya baba yangu, ´Aqiydah ya waalimu wetu, ´Aqiydah ya wale tuliokutana nao miongoni mwa wanazuoni na ´Aqiydah ya wanazuoni ambao hatukuwakuta lakini tumeletewa khabari zao. Basi yeyote atakayesema kinyume na haya, basi huyo amesema uongo.”

Abul-Hasan al-Ash´ariy amesema katika “Maqaalaat-ul-Islaamiyyiyn wa Ikhtilaaf-ul-Muswalliyn”:

“Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-ul-Hadiyth na Ahl-us-Sunnah. Miongoni mwa ´Aqiyah za Ahl-ul-Hadiyth was-Sunnah ni kumthibitisha Allaah, Malaika Wake, Mitume Yake, yote yaliyosemwa na Allaah na yale yote waliyoyapokea waaminifu kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hawarudishi chochote katika hayo.

Wanathibitisha kuwa Allaah (Subhaanah) ni mungu Mmoja ambaye kila mmoja anamuhitaji na ambaye hamuhitaji yeyote. Hakuna mungu mwingine wa haki isipokuwa Yeye. Hakujifanyia mke wala mwana.

Wanathibitisha kuwa Muhammad ni mja na Mtume Wake, kwamba Pepo ni haki, kwamba Moto ni haki na kwamba Saa haina shaka yoyote kuwa itafika na kwamba Allaah atawafufua waliyomo ndani ya makaburi.

Wanathibitisha kuwa Allaah (Subhaanah) yuko juu ya ´Arshi Yake, kama Alivosema:

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.”[2]

Na kwamba yuko na mikono miwili isiyotakiwa kufanyiwa namna, kama Alivosema:

مَا مَنَعَكَ أَن تَسْجُدَ لِمَا خَلَقْتُ بِيَدَيَّ

”Kipi kilichokuzuia usimsujudie Niliyemuumba kwa mikono Yangu?”[3]

Haya ndio jumla ya kile wanachokiamrisha, kujisalimisha nacho na kukiamini. Yale maoni yote tuliyotaja ndio ninayoona pia. Mafanikio yetu yote yako kwa Allaah na yeye ndiye Mwenye kutakwa msaada.”[4]

Ameyasema hayo pia katika “Jumal-ul-Maqaalaat” na “al-Ibaanah fiy Usuwl-id-Diyaanah”, kama alivyonakili hayo Ibn Fawrak, Ibn ´Asaakir na maimamu wengine.

Imaam Abu Bakr al-Aajurriy amesema:

”Upande mwingine wanazuoni wanasema kuwa Allaah (´Azza wa Jall) yuko juu ya ´Arshi Yake juu ya mbingu Zake. Ujuzi Wake umekizunguka kila kitu kilichoko mbinguni, ardhini na kilichoko baina yavyo. Ana ujuzi wa vya siri na vyenye kuonekana. Ana ujuzi wa utashi na fikira. Anasikia na anaona. Hakika Yeye (Subhaanah) yuko juu ya ´Arshi Yake. Kwake kunapanda matendo ya waja.”[5]

Imaam Abu Bakr al-Ismaa´iyl amesema:

”Tambua – Allaah aturehemu sisi na nyinyi – ya kwamba madhehebu ya Ahlul-Hadiyth, Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah yamejengwa juu ya kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake na kuyakubali yaliyosemwa na Qur-aan na mapokezi yaliyosihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hayatakiwi kurudishwa na wala hakuna namna ya kufanya hivo. Haya ni kwa sababu wameamrishwa kufuata Qur-aan na Sunnah. Wanaona kuwa humo mna dhamana ya uongofu na wanashuhudia ya kwamba Mtume wao (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anaongoza katika Njia iliyonyooka na wakati huohuo wanatahadhari juu ya fitina na adhabu iumizayo kwa khukhalifu viwili hivyo. Wanaitakidi kuwa Allaah anaombwa kwa majina Yake Aliyojiita nayo Mwenyewe, sifa Zake alizojisifia nazo Mwenyewe na yale majina na sifa aliyomwita na kumsifia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amemuumba Aadam kwa mikono Yake. Mikono Yake ni yenye kukunjuliwa na anatunuku Atakavyo. Hili halitakiwi kufanyiwa namna. Kadhalika (´Azza wa Jall) amelingana juu ya ´Arshi. Hili pia halitakiwi kufanyiwa namna, kwa sababu Allaah (Ta´ala) amelingana juu ya ´Arshi pasi na kuelezea namna alivyolingana.”[6]

Haafidhw Abush-Shaykh al-Aswbahaaniy amesema:

”Mlango unaozungumzia ´Arshi na Kursiy ya Mola (Tabaarak wa Ta´ala) na ukubwa wa viumbe hivi viwili pamoja na uwepo uwepo wa Mola (Tabaarak wa Ta´ala) juu ya ´Arshi Yake.”[7]

Halafu akataja Hadiyth kadha zinazofahamisha juu ya hayo.

[1] al-Haa-iyyah, uk. 45.

[2] 20:5

[3] 38:75

[4] Maqaalaat-ul-Islaamiyyiyn (1/350).

[5] ash-Shariy´ah, s. 292.

[6] I´tiqaadu A’immati Ahl-il-Hadiyth, uk. 396.

[7] al-´Adhwamah (198-201).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad bin ´Abdil-Haadiy al-Maqdisiy (afk. 744)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Kalaam ´alaa Mas-alat-il-Istiwaa’ ´alaal-´Arsh, uk. 72-74
  • Imechapishwa: 23/12/2025