19. Kuna wajibu upi juu ya Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?

´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy (rahimahullaah) amesema:

Swali 19: Kuna wajibu upi juu ya Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?

Jibu: Katika utimilifu wa kumuamini na kumpenda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kuwapenda Maswahabah zake kutokamana daraja na kutangulia kwao.

Mtu anatakiwa kukiri fadhila zao ambazo wamewashinda kwazo Ummah mzima.

Mtu anatakiwa kumuabudu Allaah kwa kuwapenda na kueneza fadhila zao.

Haifai kwa mtu kuingilia yale yaliyopitika kati yao.

Ni lazima kwetu kuamini kuwa wao wana haki zaidi ya kila sifa yenye kusifiwa kuliko walivyo wengine na kwamba wao wamewatangulia wengine wote katika kila kheri na wako mbali kabisa na kila shari.

Ni lazima kuamini kuwa wote walikuwa ni waadilifu na kwamba Allaah amewaridhia.

MAELEZO

Lililo la wajibu kwa kila muislamu atambue haki ya Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) kwa yale ambayo Allaah amewafadhilisha kwayo. Allaah amewafanya kusuhubiana na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuwasifu ndani ya Kitabu Chake sehemu nyingi katika. Amesema:

مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّهِ ۚ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّاءُ عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاءُ بَيْنَهُمْ ۖ تَرَاهُمْ رُكَّعًا سُجَّدًا يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّهِ وَرِضْوَانًا ۖ سِيمَاهُمْ فِي وُجُوهِهِم مِّنْ أَثَرِ السُّجُودِ ۚ ذَٰلِكَ مَثَلُهُمْ فِي التَّوْرَاةِ ۚ وَمَثَلُهُمْ فِي الْإِنجِيلِ كَزَرْعٍ أَخْرَجَ شَطْأَهُ فَآزَرَهُ فَاسْتَغْلَظَ فَاسْتَوَىٰ عَلَىٰ سُوقِهِ يُعْجِبُ الزُّرَّاعَ لِيَغِيظَ بِهِمُ الْكُفَّارَ

“Muhammad ni Mtume wa Allaah. Na wale walio pamoja naye ni wakali zaidi dhidi ya makafiri wanahurumiana baina yao. Utawaona wakirukuu na wakisujudu wakitafuta fadhila na radhi kutoka kwa Allaah. Alama zao dhahiri zi katika nyuso zao kutokana na athari za sujudu. Huu ndio wasifu wao katika Tawraat na wasifa wao katika Injiyl kama mmea umetoa chipukizi lake, likautia nguvu kisha likawa nene, kisha likasimama sawasawa juu ya shina lake liwapendezeshe wakulima ili liwaghadhibishe makafiri.”[1]

لِلْفُقَرَاءِ الْمُهَاجِرِينَ الَّذِينَ أُخْرِجُوا مِن دِيَارِهِمْ وَأَمْوَالِهِمْ يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانًا وَيَنصُرُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ وَالَّذِينَ تَبَوَّءُوا الدَّارَ وَالْإِيمَانَ مِن قَبْلِهِمْ يُحِبُّونَ مَنْ هَاجَرَ إِلَيْهِمْ وَلَا يَجِدُونَ فِي صُدُورِهِمْ حَاجَةً مِّمَّا أُوتُوا وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ ۚ وَمَن يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Wapatiwe pia mafuqara Muhaajiruun ambao wametolewa kutoka majumbani mwao na mali zao wanatafuta fadhilah na radhi kutoka kwa Allaah na wanamnusuru Allaah na Mtume Wake – hao ndio wakweli. Na wale waliokuwa na makazi [Madiynah] na wakawa na imani kabla yao wanawapenda wale waliohajiri kwao na wala hawahisi choyo yoyote vifuani mwao kwa yale waliyopewa [Muhaajiruun] na wanawapendelea kuliko nafsi zao japokuwa wao wenyewe ni wahitaji. Na yeyote anayeepushwa na uchu wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufaulu.” Na wale waliokuja baada yao wanasema: Rabb wetu! Tughufurie na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa iymaan na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini; Rabb wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.”[2]

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا عَدُوِّي وَعَدُوَّكُمْ أَوْلِيَاءَ تُلْقُونَ إِلَيْهِم بِالْمَوَدَّةِ وَقَدْ كَفَرُوا بِمَا جَاءَكُم مِّنَ الْحَقِّ يُخْرِجُونَ الرَّسُولَ وَإِيَّاكُمْ ۙ أَن تُؤْمِنُوا بِاللَّـهِ رَبِّكُمْ إِن كُنتُمْ خَرَجْتُمْ جِهَادًا فِي سَبِيلِي وَابْتِغَاءَ مَرْضَاتِي ۚ تُسِرُّونَ إِلَيْهِم بِالْمَوَدَّةِ وَأَنَا أَعْلَمُ بِمَا أَخْفَيْتُمْ وَمَا أَعْلَنتُمْ ۚ وَمَن يَفْعَلْهُ مِنكُمْ فَقَدْ ضَلَّ سَوَاءَ السَّبِيلِ

”Enyi mlioamini! Msimfanye adui Wangu na adui wenu marafiki wandani mkiwapelekea [siri za mikakati] kwa mapenzi na hali wamekwishakanusha haki iliyokujieni. Wanamtoa kwa kumfukuza Mtume pamoja na nyinyi kwa vile tu mmemuamini Allaah, Mola wenu; ikiwa mmetoka kwa ajili ya Jihaad katika njia Yangu na kutafuta radhi Zangu. Mnawapa siri kwa mapenzi na hali Mimi najua yale mnayoyaficha na yale mnayoyadhihirisha. Na yeyote yule atakayefanya hivyo katika nyinyi, basi hakika amepotea njia ya sawa.”[3]

لَّقَد تَّابَ اللَّـهُ عَلَى النَّبِيِّ وَالْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ الَّذِينَ اتَّبَعُوهُ فِي سَاعَةِ الْعُسْرَةِ مِن بَعْدِ مَا كَادَ يَزِيغُ قُلُوبُ فَرِيقٍ مِّنْهُمْ ثُمَّ تَابَ عَلَيْهِمْ ۚ إِنَّهُ بِهِمْ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Hakika Allaah amepokea tawbah ya Nabii na Muhajiruun na Answaar ambao wamemfuata katika saa ya dhiki baada ya nyoyo za kundi miongoni mwao zilikaribia kupondoka kisha akapokea tawbah yao. Hakika Yeye kwao ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.”[4]

Zipo Aayah nyingi ambazo Allaah amewasifu Maswahabah wa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akathibitisha uadilifu wao na akapitisha kuwa wao ndio bora kuliko watu wengine wote mbali na Mitume. Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Watu bora ni wa karne yangu. Kisha wale watakaofuatia, kisha wale watakaofuatia. Kisha watakuja watu ambao ushuhuda wao unatangulia viapo vyao  na viapo vyao vinatangulia ushuhuda wao.”[5]

Bi maana watakuwa na haraka ya kushuhudia na kula yamini kabla ya kuombwa kufanya hivo.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kuwatukana Maswahabah wake na akasema:

“Msiwatukane Maswahabah wangu. Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi ya Muhammad imo mikononi Mwake lau mmoja wenu atajitolea dhahabu mfano wa mlima wa Uhud basi hatofikia viganja viwili vya mikono vilivyojazwa na mmoja wao wala nusu yake.”[6]

Alisema hivo wakati kulipotokea tofauti kidogo kati ya ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf na Khaalid bin al-Waliyd. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa amemtuma Khaalid kwenda kwa Banu Judhaymah aliyowaua. Akawachomolea upanga ambapo wakasema: “Tumeteremka chini!” Hawakujua kuwa wanatakiwa kusema: “Tumesilimu!” ´Abdur-Rahmaan akamkataza kuwaua, lakini akaendelea kung´ang´ania kuwaua. Ndipo Khaalid akasema kumwambia: “Hamjifakharishi juu yetu isipokuwa tu kwa baadhi ya siku ambazo mmeingia ndani ya Uislamu kabla yetu.” Wakati waliporejea kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ´Abdur-Rahmaan alimshtaki Khaalid bin al-Waliyd ndipo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema maneno ambayo punde tumeyataja.

Ikiwa haya yalisemwa juu ya Swahabah aliyekuja nyuma kwa sababu ya Swahabah aliyetangulia mbele, tusemeje juu ya yule ambaye hayuko hata karibu na Maswahabah na bali akafikia mpaka kuwatukana Maswahabah? Kwa hiyo ni lazima kwa kila muislamu atambue fadhilah za Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na awape haki zao kwa kuwaadhimisha, kuwatukuza na kuwaheshimisha.

Jengine ni kwamba anatakiwa kufunga mdono wake kutokamana na yale yaliyopitika baina yao. Mtunzi wa kitabu amesema:

“Ni lazima kwetu kuamini kuwa wao wana haki zaidi ya kila sifa yenye kusifiwa kuliko walivyo wengine na kwamba wao wamewatangulia wengine wote katika kila kheri na wako mbali kabisa na kila shari.”

Allaah awalaani Raafidhwah wanaomtukana Abu Bakr, ´Umar, ´Uthmaan na Maswahabah wengine waliobaki. Allaah awalaani. Tunamuomba Allaah awatweze. Amewatweza kwa kule kuwaacha kwao katika imani hii mbaya ambayo watakutana kwayo na ghadhabu na hasira za Allaah. Ni wenye kuwatukana mno Maswahabah wabora kama mfano wa Abu Bakr, ´Umar, ´Uthmaan, ´Aaishah na Hafswah (Radhiya Allaahu ´anhum). Bali wana mazowea majibwa na punda wao kuwapa jina la Abu Bakr na ´Umar. Wanadai kuwa wanampenda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na watu wa nyumbani kwake. Wamesema uongo. Lau kweli wangelikuwa wanampenda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi wasingelisema juu ya Maswahabah maneno hayo mabaya.

Ni lazima kwetu kutambua fadhilah za wale wenye fadhilah katika wao. Tunamtanguliza Abu Bakr, ´Umar, ´Uthmaan na ´Aliy juu ya wengine wote (Radhiya Allaahu ´anhum). Kisha wanafuata wale Maswahabah kumi ambao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekufa hali ya kuwa radhi na wao na akaeleza kuwa ni watu wa Peponi. Halafu wale waliohajiri mara mbili: mara ya kwanza kwenda Uhabeshi na mara ya pili kwenda Madiynah. Kisha wale walioshuhudia Badr. Kisha wale waliokula kiapo chini ya mti. Halafu wale walioingia katika Uislamu na wakapambana kabla ya kufunguliwa mji wa Makkah. Kisha wale walioingia katika Uislamu baada ya kufunguliwa mji wa Makkah na wakapambana. Halafu wale Maswahabah wadogo na kadhalika.

Maswahabah wote ni waadilifu kwa kule Allaah kuwafanya kuwa ni waadilifu. Ummah umeafikiana juu ya hilo. Pindi Hadiyth inaposilimuwa na Swahabah basi hakuulizwi juu ya uadilifu wa Swahabah huyo. Kwa sababu Allaah ndiye amewafanya kuwa waadilifu.

Tunamuomba Allaah atujaalie kuwa miongoni mwa wale wenye kutambua haki za Maswahabah wa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), tukawasifu kwa ndimi na kuzieneza sifa zao nzuri.

[1] 48:29

[2] 59:08-09

[3] 60:1

[4] 09:117

[5] al-Bukhaariy (2652) na Muslim (2533).

[6] al-Bukhaariy (3673) na Muslim (2541).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyaat ´alaa Kitaab Ahamm-il-Muhimmaat, uk. 102-105
  • Imechapishwa: 26/10/2021