84 – al-Husayn bin Mansuur bin Ja´far ametukhabarisha: Abu Usaamah ametukhabarisha: Hishaam bin ´Urwah ametukhabarisha, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Asmaa’ bint Abiy Bakr, aliyesimulia:

“Nilimuona Zayd bin ‘Amr bin Nufayl akiwa amesimama hali ya kuegemeza mgongo wake kwenye Ka’bah na kusema: “Hakuna yeyote katika nyinyi leo hii aliye juu ya dini ya Ibraahiym zaidi yangu. Alikuwa akisema: “Mungu wangu ni mungu wa Ibraahiym na dini yangu ni dini ya Ibraahiym.” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alimtaja na kusema: “Siku ya Qiyaamah atamfufua yeye kama ummah wa kujitegemea, baina yangu na ´Iysaa.”[1]

85 – Muusa bin Hizaam ametukhabarisha: Abu Usaamah ametukhabarisha, kutoka kwa Muhammad bin ´Amr, kutoka kwa Abu Salamah bin ´Abdir-Rahmaan na Yahyaa bin ´Abdir-Rahmaan bin Haatib, kutoka kwa Usaamah bin Zayd, kutoka kwa Zayd bin Haarithah, ambaye amesema:

“Siku moja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alifuatana nami kwenye machinjio fulani. Tukamchinjia mwana-kondoo na tukampikia. Ilipokamilika tuliiweka kwenye turubai yetu. Kisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akaendelea na safari yake nyuma yangu katika siku ya Makkah yenye joto. Tulipofika sehemu ya juu ya bonde, alikutana na Zayd bin ‘Amr bin Nufayl. Wakasalimiana kwa salamu za kabla ya kuja Uislamu ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia: “Inakuweje watu wako wanakudharau?” Alisema: “Kwa sababu ya ugomvi uliokuwepo kati yangu na wao. Hata hivyo mimi nawaona wako kwenye upotofu. Nikaondoka kuitafuta dini hii na nikafika kwa marabi wa Yathrib, lakini nikawakuta wanamwabudu Allaah na wanamshirikisha, nikasema hiyo si dini ninayoitafuta. Kisha nikaondoka mpaka nilipofika kwa marabi wa Khaybar, lakini nikawakuta wakimuabudu Allaah na wanamshirikisha, nikasema kuwa hii si dini ninayoitaka. Kisha nikaondoka mpaka nilipofika kwa marabi wa Fadak, lakini nikawakuta wakimuabudu Allaah na wanamshirikisha, nikasema kuwa hii si dini ninayoitaka. Kisha nikaondoka mpaka nilipofika kwa marabi wa Ayla, nikawakuta wakimuabudu Allaah na wanamshirikisha, nikasema kuwa hii si dini ninayoitaka. Rabi mmoja wa Shaam akanambia: “Je, unauliza juu ya dini ambayo kutokana na ninavyojua hakuna yeyote anayemwabudu Allaah kwayo isipokuwa mzee mmoja katika kisiwa cha waarabu?” Nikaondoka, nikamwendea, nikamweleza kusudio langu. Akasema: “Kila niliyemwona yuko kwenye upotofu. Hakika wewe unauliza juu ya dini ambayo ni dini ya Allaah na Malaika wake. Kwenye nchi yako atakuja Nabii ambaye atalingania juu yake. Rudi,  umsadikishe, umfuate na uyaamini yale aliyokuja nayo.” Bado hajakutana na Nabii yeyote. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamfanya yule ngamia aliyekuwa chini yake kupiga magoti. Kisha tukamkaribisha meza iliyokuwa na nyama choma. Akasema, “Hii ni nini?” Tukasema, Huyu ni mwana-kondoo tuliyemchinja kwenye machinjio fulani.” Ndipo akasema: “Sili chochote kilichochinjwa kwa ajili ya Allaah.” Baada ya hapo kila mmoja akashika njia yake. Kulikuwa na masanamu wawili wa shaba wanaoitwa Isaaf na Naa-ilah. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akatufu nami nikatufu naye. Nilipopita karibu nalo nikalipapasa ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema: “Usilipapase.” Tukaenelea kutufu. Nikajiambia mwenyewe kwamba nitalipapasa tena na kuona nini atachosema, ambapo nikafanya hivo. Alisema: “Usilipapase. Si umeshakatazwa?” Naapa kwa Aliyemtukuza na akamteremshia Kitabu! Tangu wakati huo sikupapasa tena sanamu yoyote mpaka pale Allaah alipomtukuza na kumteremshia Kitabu.” Zayd bin ‘Amr bin Nufayl alikufa kabla ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kutumilizwa. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: “Siku ya Qiyaamah atamfufua yeye kama ummah wa kujitegemea.”[2]

86 – Ahmad bin Sulaymaan ametukhabarisha: ´Affaan ametukhabarisha: Wuhayb ametukhabarisha: Muusa bin ´Uqbah amenihadithia: Saalim ametukhabarisha kuwa amemsikia ´Abdullaah bin ´Umar akieleza:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikutana na Zayd bin ´Amr kwenye Baldah ya chini kabla ya kuteremshiwa wahy ambapo akamkaribisha kwenye meza iliyokuwa na nyama. Akakataa kula na akasema: “Sili chochote mnachochinja juu ya masanamu yenu, wala sili isipokuwa kile hakikutajiwa jina la Allaah[3].”[4]

Haya yamesimuliwa na ´Abdullaah bin ´Umar kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

[1] al-Bukhaariy (3614).

[2] adh-Dhahabiy amesema:

“Kwenye cheni ya wapokezi yuko Muhammad, ambaye hawezi kutumiwa kama hoja. Isitoshe Hadiyth iko na mgongano wa wazi.” (Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (1/222))

[3] al-Albaaniy amesema:

“Zayd alifikiri kuwa nyama hiyo aliyokaribishwa ni miongoni mwa zile nyama ambazo Allaah kaharamisha. Ndio maana nyumba ya Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) hawakula nyama iliyoandaliwa kwa ajili ya masanamu, lakini alitaka kuhakikisha na kuweka hadharani imani yake. Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) hakulisahau hilo, bali akafurahishwa nalo.” ( Fiqh-us-Siyrah, uk. 65)

[4] al-Bukhaariy (5499).

  • Muhusika: Imaam Ahmad bin Shu´ayb an-Nasaa’iy (afk. 303)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwaa-il-us-Swahaabah, uk. 72-75
  • Imechapishwa: 09/09/2026