188. Namna hii ndio mtu hujisababishia kuingia Pepo au Motoni

Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

142 – Allaah (Ta´ala) ameumba Pepo na Moto kabla ya kuumba vitu vyengine. Aidha akaviumbia wakazi wake. Yule ambaye Anamtaka ataingia Peponi, atafanya hivo kutokana na fadhilah Zake, na yule ambaye Anamtaka ataingia Motoni, atafanya hivo kutokana na uadilifu Wake. Kila mmoja anatenda kwa yale ambayo amekwishakadiriwa na anapita juu ya yale aliyoumbiwa kwayo.

MAELEZO

Allaah amewaumbia Pepo wakazi wake na amewaumbia Moto wakazi wake, na kila mmoja analipwa kutegemea matendo yake. Pepo haipatikani kwa matendo; matendo ni sababu tu inayopelekea kuipata Pepo. Pepo inapatikana kutokana na fadhilah zake Allaah. Vovyote ambavo mwanadamu atafanya katika matendo mema, hayalingani na kuipata Pepo. Pepo inapatikana kwa fadhilah  za Allaah (´Azza wa Jall). Matendo mema ni sababu tu ya kuipata Pepo:

ادْخُلُوا الْجَنَّةَ بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ

“ingieni Peponi kwa yale mliyokuwa mkitenda.”[1]

Bi maana kwa sababu ya yale mliyokuwa mkifanya.

Kuingia Moto ni kwa sababu ya ukafiri. Hilo ni uadilifu wa Allaah. Allaah amemwingiza mtu Motoni kwa uadilifu na si dhuluma. Ameingia humo kwa sababu ya matendo yake mwenyewe.

Akiwa ni miongoni mwa watu wenye furaha, basi atafanya matendo wa watu wenye furaha. Na akiwa ni miongoni mwa watu waliokula khasara, basi atafanya matendo wa watu waliokula khasara. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Fanyeni matendo! Hakika kila mmoja amefanyiwa wepesi kwa yale aliyoumbiwa.”[2]

Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ سَعْيَكُمْ لَشَتَّى فَأَمَّا مَن أَعْطَى وَاتَّقَى وَصَدَّقَ بِالْحُسْنَى فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْيُسْرَى وَأَمَّا مَن بَخِلَ وَاسْتَغْنَى  وَكَذَّبَ بِالْحُسْنَى فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْعُسْرَى

“Hakika juhudi zenu bila shaka ni zenye kutofautiana. Basi yule anayetoa na akamcha Allaah na akasadikisha lililo jema zaidi, basi tutamuwepesishia kwa yaliyo mepesi. Ama yule afanyaye ubakhili na akajiona amejitosheleza na akakadhibisha lililo jema zaidi, basi tutamuwepesishia kwa yaliyo magumu.”[3]

Matendo ndio yatayokuhukumu; yakiwa mema, basi yatakusahilishia mepesi, na yakiwa maovu, yatakusahilishia magumu.

[1]16:32

[2]al-Bukhaariy (4949) na Muslim (2647).

[3]92:4-10

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 205-206
  • Imechapishwa: 29/03/2025