Thawabu juu ya yale matendo mema, adhabu juu ya yale matendo maovu.

Njia ni daraja itayowekwa juu ya Moto. Njia hiyo ina makali zaidi kushinda upanga, nyembamba zaidi kushinda nywele, yenye moto zaidi kuliko mkaa. Watu watapita juu yake kutokana na matendo yao. Wako ambao watapita kama umeme, wengine watapita kama upepo, wengine watapita kama farasi waendao mbio na ngamia, wengine watapita kwa kukimbia, wengine watapita kwa kutembea na wengine watapita kwa kutambaa. Wengine watashikwa na ndoano na kutupwa ndani ya Moto. Haya ni mambo ya ghaibu, kwa ajili hiyo haitakikani kwa mtu akayapekua kutokana na akili yake. Kila mtu atapita juu ya Moto:

وَإِن مِّنكُمْ إِلَّا وَارِدُهَا ۚ كَانَ عَلَىٰ رَبِّكَ حَتْمًا مَّقْضِيًّا ثُمَّ نُنَجِّي الَّذِينَ اتَّقَوا وَّنَذَرُ الظَّالِمِينَ فِيهَا جِثِيًّا

“Hakuna yeyote miongoni mwenu isipokuwa ataufikia. Hiyo kwa Mola wako ni hukumu ya lazima kutimizwa. Kisha tutawaokoa wale waliomcha Allaah na tutawaacha madhalimu humo wamepiga magoti.”[1]

Matendo mema yatapimwa kwenye mzani. Yule ambaye mema yake yatashinda uzito maovu yake, basi atafuzu, na yule ambaye maovu yake yatashinda uzito mema yake, atakhasirika:

وَالْوَزْنُ يَوْمَئِذٍ الْحَقُّ ۚ فَمَن ثَقُلَتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ وَمَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُم بِمَا كَانُوا بِآيَاتِنَا يَظْلِمُونَ

“Kipimo kwa mizani siku hiyo itakuwa ni haki, basi ambao mizani yao itakuwa nzito, hao ndio watakaofaulu na ambao mizani yao itakuwa khafifu, basi hao ni wale waliokhasirika nafsi zao kwa yale waliyokuwa wakizifanyia dhuluma Aayah Zetu.”[2]

Jambo la kupimwa na mizani limetajwa mara nyingi ndani ya Qur-aan, kitu ambacho kinafahamisha uadilifu wa Allaah (´Azza wa Jall). Hamdhulumu yeyote. Ni mizani ya kikweli. Mizani hiyo iko na masahani mawili. Matendo mema yatawekwa katika sahani moja na maovu yatawekwa katika sahani lingine. Ambaye mema yake ndio yatakuwa na uzito zaidi, atafaulu, ambaye maovu yake ndio yatakuwa na uzito zaidi, amekula khasara:

وَنَضَعُ الْمَوَازِينَ الْقِسْطَ لِيَوْمِ الْقِيَامَةِ فَلَا تُظْلَمُ نَفْسٌ شَيْئًا ۖ وَإِن كَانَ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ أَتَيْنَا بِهَا ۗ وَكَفَىٰ بِنَا حَاسِبِينَ

“Tutaweka mizani ya uadilifu siku ya Qiyaamah – hivyo nafsi haitodhulumiwa kitu chochote japo ikiwa uzito wa mbegu ya hardali Tutaileta. Inatosheleza Kwetu kuwa wenye kuhesabu.”[3]

[1]19:71-72

[2]7:8-9

[3]21:47

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 202-203
  • Imechapishwa: 29/03/2025