Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab amesema:

Nguzo ya pili ni kusoma “al-Faatihah” nayo ni nguzo katika kila Rakaa´. Kama ilivyo katika Hadiyth:

“Hana swalah kwa yule asiyesoma ufunguzi wa kitabu.”[1]

Nayo ndiyo mama wa Qur-aan.

بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

”Kwa jina la Allaah, Mwingi wa huruma, Mwenye kurehemu.”

Ni baraka na kinga.

الْحَمْدُ للّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

”Himdi zote njema anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu.”[2]

Himdi ni sifa. Kule kutajwa kwa njia iliyoanishwa (ال) inafahamisha kukusanya himdi zote. Ama kizuri ambacho hakikujifanya, kama mfano wa uzuri na mfano wake, kinatapwa na hakisifiwi.

Mola ni Mwabudiwa, Muumba, Mwenye kuruzuku, Mfalme, Anayevisimamia na kuvilea viumbe vyote kwa neema Zake.

Mola wa walimwengu ni kila kisichokuwa Allaah. Naye ni Mola wa walimwengu.

الرَّحْمنِ الرَّحِيمِ

“Mwingi wa huruma, Mwenye kurehemu.”[3]

Mwingi wa huruma ni huruma unaowapata viumbe wote.

Mwenye kurehemu ni huruma maalum kwa waumini. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَكَانَ بِالْمُؤْمِنِينَ رَحِيمًا

“Naye daima ni Mwenye kuwarehemu waumini.”[4]

مَلِكِ يَوْمِ الدِّينِ

”Mfalme wa siku ya Qiyaamah!”[5]

Ni siku ya malipo na hesabu. Siku ambayo kila mmoja atalipwa kwa matendo yake. Kama ni mema malipo yatakuwa mema, na kama ni shari malipo yatakuwa shari. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَمَا أَدْرَاكَ مَا يَوْمُ الدِّينِ ثُمَّ مَا أَدْرَاكَ مَا يَوْمُ الدِّينِ يَوْمَ لَا تَمْلِكُ نَفْسٌ لِّنَفْسٍ شَيْئًاۖ وَالْأَمْرُ يَوْمَئِذٍ لِّلَّـهِ

”Ni kipi kitakachokujulisha siku ya malipo? Kisha nini kitakachokujulisha siku ya malipo? Siku ambayo nafsi haitomiliki chochote juu ya nafsi nyingine na amri siku hiyo ni ya Allaah pekee.”[6]

Hadiyth kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye akili ni yule ambaye anaibidisha nafsi yake na kufanyia kazi kwa yanayomgonja baada ya mauti na asiye muweza ni yule ambaye anafuata matamanio ya nafsi yake na huku akiwa na matumaini ya uongo kwa Allaah.”[7]

إِيَّاكَ نَعْبُدُ

”Wewe pekee ndiye tunakuabudu… ”[8]

Yaani hatumuabudu mwengine yeyote badala Yako. Hii ni ahadi iliopo baina ya mja na Mola Wake ya kwamba hatomuabudu mwengine asiyekuwa Yeye.

وإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

“… na Wewe pekee ndiye tunakutaka msaada.”[9]

Yaani ni ahadi iliopo baina ya mja na Mola Wake kwamba hatoomba msaada kwa mwengine asiyekuwa Yeye.

اهدِنَا الصِّرَاطَ المُستَقِيمَ

“Tuongoze katika njia iliyonyooka… ”[10]

Yaani tuongoze, utuelekeze na ututhibitishe. Njia ni Uislamu. Imesemekana pia kuwa ni Mtume na wengine wakasema kuwa ni Qur-aan. Maana zote hizi ni haki. Iliyonyooka ni ile ambayo isiyokuwa na upindaji wowote ndani yake.

صِرَاطَ الَّذِينَ أَنعَمتَ عَلَيهِمْ

”… njia ya wale uliyowaneemeshe.”[11]

Njia ya wale uliyowaneemeshe. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَمَن يُطِعِ اللّهَ وَالرَّسُولَ فَأُوْلَئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللّهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاء وَالصَّالِحِينَ وَحَسُنَ أُولَئِكَ رَفِيقًا

“Atakayemtii Allaah na Mtume basi hao watakuwa pamoja na wale Allaah aliowaneemesha – Manabii na wakweli na mashahidi na waja wema – na uzuri ulioje kuwa na tangamano kama hili!”[12]

غَيرِ المَغضُوبِ عَلَيهِمْ

”… si ya wale Uliowaghadhibikia… ”

Walioghadhibikiwa nao ni mayahudi waliopewa elimu pasi na kuitendea kazi. Tunamuomba Allaah Atukinge na njia yao.

وَلاَ الضَّالِّينَ

”… na wala wale waliopotea!”

Waliopotea nao ni manaswara wanaomuabudu Allaah kwa ujinga na upotevu. Tunamuomba Allaah Atukinge na njia zao. Dalili ya waliopotea ni Kauli Yake (Ta´ala):

قُلْ هَلْ نُنَبِّئُكُمْ بِالْأَخْسَرِينَ أَعْمَالًا الَّذِينَ ضَلَّ سَعْيُهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ يَحْسَبُونَ أَنَّهُمْ يُحْسِنُونَ صُنْعًا

“Sema: “Je, Tukujulisheni ni wepi ambao matendo yao yamekhasirika? Ni wale ambao wamepoteza juhudi zao katika uhai wa dunia nao wakidhani kwamba wanatenda vizuri.”[13]

Kadhalika amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mtafuata nyenendo za waliokuwa kabla yenu shibri kwa shibri na pima kwa pima hata wakiingia katika shimo la mburukenge mutaingia nao.” Wakauliza: “Je, unakusudia mayahudi na manasara?” Akasema: “Ni nani wengine ikiwa si wao?”[14]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Hadiyth nyingine inasema:

“Wamegawanyika mayahudi katika mapote sabini na moja, wakagawanyika manaswara katika mapote sabini na mbili na Ummah wangu utagawanyika mapote sabini na tatu – yote hayo yataingia Motoni ila moja tu.” Maswahabah wakauliza: “Ni lipi hilo, ewe Mtume wa Allaah?” Akasema: “Ni lile litalokuwa katika mfano wa yale niliyomo mimi na Maswahabah zangu.”[15]

MAELEZO

Halafu amtaje Allaah na kusema:

بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

”Kwa jina la Allaah, Mwingi wa huruma, Mwenye kurehemu.”

Hali ya kumtaka msaada Allaah.

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ni Yule mwenye kuabudiwa na viumbe wote.

Mwingi wa huruma na Yule ambaye ana rehema zilizoenea.

Mwenye kurehemu ni rehema maalum kwa waumini:

وَكَانَ بِالْمُؤْمِنِينَ رَحِيمًا

“Naye daima ni Mwenye kuwarehemu waumini.”

إِنَّ اللَّـهَ بِالنَّاسِ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ

”Hakika Allaah kwa watu ni Mwenye huruma sana, Mwenye kurehemu. [16]

الْحَمْدُ للّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

”Himdi zote anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu.”

Himdi ni sifa kama tulivosema. Mola wa walimwengu ni Mola wa viumbe wote.

الرَّحْمنِ الرَّحِيمِ

“Mwingi wa huruma, Mwenye kurehemu.”

Mwingi wa huruma ni Mwenye huruma ulioenea. Mwenye kurehemu ni Mwenye huruma maalum kuwarehemu waumini peke yao.

 مَلِكِ يَوْمِ الدِّينِ

”Mfalme wa siku ya malipo!”

Siku ya malipo na hesabu. Yeye ndiye mmiliki wa siku ya malipo na siku ya hesabu. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا أَدْرَاكَ مَا يَوْمُ الدِّينِ ثُمَّ مَا أَدْرَاكَ مَا يَوْمُ الدِّينِ يَوْمَ لَا تَمْلِكُ نَفْسٌ لِّنَفْسٍ شَيْئًاۖ وَالْأَمْرُ يَوْمَئِذٍ لِّلَّـهِ

”Ni kipi kitakachokujulisha siku ya malipo? Kisha nini kitakachokujulisha siku ya malipo? Siku ambayo nafsi haitomiliki chochote juu ya nafsi nyingine na amri siku hiyo ni ya Allaah pekee.”[17]

Katika Hadiyth imekuja:

Hadiyth kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye akili ni yule ambaye anaibidisha nafsi yake na kufanyia kazi kwa yanayomgonja baada ya mauti na asiye muweza ni yule ambaye anafuata matamanio ya nafsi yake na huku akiwa na matumaini ya uongo kwa Allaah.”

Mwenye akili ni yule anayeifanyia hesabu nafsi yake mwenyewe na akajibidisha kwa ajili ya Aakhirah. Asiye muweza ni yule ambaye anafuata matamanio ya nafsi yake na huku akiwa na matumaini ya uongo kwa Allaah. Hadiyth ni yenye kutambulika. Katika cheni ya wapokezi wake kuna udhaifu fulani.

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

”Wewe pekee ndiye tunakuabudu na Wewe pekee ndiye tunakutaka msaada.”

Pekee yako, ee Mola, ndiye tunakuabudu na kukutekelezea ´ibaadah. ´Ibaadah inahusiana na kutekeleza yale yote aliyoamrisha kukiwemo swalah na swawm. Wewe pekee ndiye tunakutaka msaada juu ya mambo yetu ya kidunia. Wewe pekee, ee Mola, ndiye tunakutaka msaada katika kila kitu. Ni dalili inayofahamisha kwamba mja anatakiwa kumuabudu na kumtaka msaada Mola wake pekee. Hivo ndo sahihi. Kwa hiyo ni wajibu kwa mja amtekelezee ´ibaadah Allaah pekee. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَادْعُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ وَلَوْ كَرِهَ الْكَافِرُونَ

”Basi mwombeni Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini japokuwa wanachukia makafiri.” [18]

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

”Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu ambaye amekuumbeni na wale waliokuwa kabla yenu mpate kucha.”[19]

اهدِنَا الصِّرَاطَ المُستَقِيمَ

“Tuongoze katika njia iliyonyooka… ”

Tuongoze, utuelekeze na ututhibitishe katika njia iliyonyooka. Uongofu maana yake ni kuonyesha, maelekezo na uthibitisho. Njia iliyonyooka ni njia ambayo Allaah amewawekea katika Shari´ah waja Wake na akaifanya ni yenye kumfikia. Ndio njia Yake iliyonyooka ambayo amemtumiliza kwayo Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Njia iliyonyooka ni ile isiyokuwa na kupinda ndani yake na ni kule kufuata Qur-aan na Sunnah.

صِرَاطَ الَّذِينَ أَنعَمتَ عَلَيهِمْ

”… njia ya wale uliyowaneemeshe.”

Ni Mitume na wasomi wao na wafuasi wao watenda kazi. Wako katika njia iliyonyooka, njia ya wale walioneemeshwa. Ni wale watu waliojua na wakatendea kazi. Amesema (Subhaanah):

وَمَن يُطِعِ اللّهَ وَالرَّسُولَ فَأُوْلَئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللّهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاء وَالصَّالِحِينَ وَحَسُنَ أُولَئِكَ رَفِيقًا

“Atakayemtii Allaah na Mtume basi hao watakuwa pamoja na wale Allaah aliowaneemesha – Manabii na wakweli na mashahidi na waja wema – na uzuri ulioje kuwa na tangamano kama hili!”

Hawa ndio walioneemeshwa; Mitume na wafuasi wao.

غَيرِ المَغضُوبِ عَلَيهِمْ

”… si ya wale Uliowaghadhibikia… ”

Ni mayahudi. Ghadhabu za Allaah ziliwapata kwa sababu ya kufuru, hasadi na uadui wao.

وَلاَ الضَّالِّينَ

”… na wala wale waliopotea!”

Ni manaswara. Wanaabudu kwa ujinga.

Mayahudi ugonjwa wao ni ukaidi japokuwa wanajua. Manawara ugonjwa wao ni ujinga. Hii ndio hali zao mara nyingi. Amesema (Ta´ala):

قُلْ هَلْ نُنَبِّئُكُمْ بِالْأَخْسَرِينَ أَعْمَالًا الَّذِينَ ضَلَّ سَعْيُهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ يَحْسَبُونَ أَنَّهُمْ يُحْسِنُونَ صُنْعًا

“Sema: “Je, Tukujulisheni ni wepi ambao matendo yao yamekhasirika? Ni wale ambao wamepoteza juhudi zao katika uhai wa dunia nao wakidhani kwamba wanatenda vizuri.”

Hivi ndivo walivyoeleza manaswara. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtafuata nyenendo za waliokuwa kabla yenu shibri kwa shibri na pima kwa pima hata wakiingia katika shimo la mburukenge mutaingia nao.” Wakauliza: “Je, unakusudia mayahudi na manasara?” Akasema: “Ni nani wengine ikiwa si wao?”

Bi maana watu waliopatwa na ghadhabu na upotevu. Watu wengi wamefuata njia pindi walipoiacha haki na wakafuata matamanio. Mara wamefanya kwa kukusudia, mara wamefanya kwa ujinga. Amesema (Ta´ala):

وَمَا أَكْثَرُ النَّاسِ وَلَوْ حَرَصْتَ بِمُؤْمِنِينَ

“Na wengi wa watu hawatoamini japokuwa utalipupia hilo.” [20]

وَقَلِيلٌ مِّنْ عِبَادِيَ الشَّكُورُ

”Ni wachache miongoni mwa waja Wangu wenye kushukuru.” [21]

Katika Hadiyth nyingine Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mayahudi wamefarikiana katika makundi sabini na moja. Manaswara wamefarikiana katika makundi sabini na mbili. Na Ummah huu utafarikiana katika makundi sabini na tatu. Yote yataingia Motoni isipokuwa moja tu.” Wakasema: ”Ni wepi hao, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: ”Ni wale wanaofuata yale niliyomo mimi hii leo na Maswahabah zangu.”

Hali kadhalika mayahudi; waligawanyika makundi sabini na moja ambapo yote yataingia Motoni isipokuwa moja tu. Hawa ni wale wafuasi wa Muusa (´alayhis-Salaam) katika wakati wake na baada yake. Ama yaliyobaki yote ni yenye kuangamia. Vivyo hivyo manaswara; waligawanyika makundi sabini na mbili ambapo yote yataingia Motoni isipokuwa moja tu. Hawa ni wale wafuasi wa ´Iysaa na Muusa (´alayhimaas-Salaam); wafuasi wa Mitume. Yaliyobaki mengine yote yataingamia. Katika Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wataookoka ni wafuasi wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika wakati wake na baada ya kufa kwake. Ama wale wengine wote waliokwenda kinyume naye ni wenye kuangamia.

[1] al-Bukhaariy (756) na Muslim (394).

[2] 01:01

[3] 01:02

[4] 33:43

[5] 01:03

[6] 82:17-19

[7] at-Tirmidhiy (2459) aliyesema ni nzuri, Ibn Maajah (4260), Ahmad (17123) na al-Haakim (1/57) ambaye ameisahihisha. Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwa´iyf Sunan at-Tirmidhiy” (263).

[8] 01:05

[9] 01:05

[10] 01:06

[11] 01:07

[12] 04:69

[13] 18:103-104

[14] al-Bukhaariy (4356) na Muslim (2669).

[15] Ibn Maajah (3992), at-Tirmidhiy (2641) na Abu Daawuud (4596). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Mishkaat-ul-Maswaabiyh” (171).

[16] 2:143

[17] 82:17-19

[18] 40:14

[19] 2:21

[20] 12:103

[21] 34:13

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ash-Sharh al-Mumtaaz, uk. 102-106
  • Imechapishwa: 15/07/2018