18. Hakuna kheri kwa mtu asiyeelewa maana ya Shahaadah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Ukishajua ya kwamba makafiri wajinga walijua hilo, jambo la kushangaza ni kwa yule anayedai Uislamu na yeye hajui maana ya neno hili jambo ambalo walikuwa wanalijua makafiri. Badala yake anafikiria ya kwamba maana yake ni kutamka herufi zake bila ya kuamini maana yake moyoni. Mjuzi katika wao anafikiria ya kwamba maana yake ni kwamba hakuna mwenye kuumba, wala mwenye kuruzuku wala mwenye kuendesha mambo isipokuwa Allaah. Hakuna kheri kwa mtu ikiwa wajinga makafiri wanajua zaidi yake maana ya “hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah”.

MAELEZO

Bi maana walikuwa wanajua kuwa kwamba “hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah” maana yake ni hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah.

Hapa anachotaka mtunzi (Rahimahu Allaah) ni kuonyesha kuwa kuna watu wanaosema kuwa eti wao ni waislamu lakini hata hivyo hawajui maana ya “hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah”. Badala yake wanadhani kuwa inahusiana tu kutamka herufi zake pasi na kujua wala kuamini maana yake.

Kuna watu wanaodhani kuwa maana yake ni Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah, nayo ni hakuna mwenye kuumba wala mwenye kuruzuku isipokuwa Allaah.

Kuna wengine wanaifasiri “ni kuondosha yakini juu ya vitu na badala yake mtu awe na yakini ya kweli juu ya dhati ya Allaah”. Tafsiri hii ni batili na haijulikani kwa Salaf. Haina maana ya kuwa na yakini juu ya dhati ya Allaah (´Azza wa Jall) na kutokuwa na yakini juu ya kitu kingine. Hili ni jambo lisilowezekana kwa sababu mtu unaweza kuwa na yakini juu ya kitu kingine:

لَتَرَوُنَّ الْجَحِيمَ مَّ لَتَرَوُنَّهَا عَيْنَ الْيَقِينِ

“Bila shaka mtauona [Moto wa] al-Jahiym. Kisha kwa hakika mtauona [huo Moto] kwa jicho la yakini.” (102:06-07)

Kuwa na yakini juu ya mambo na vitu vinavyojulikana ni jambo lisilopingana na Tawhiyd.

Kuna wengine wanaifasiri kuwa maana yake ni “hakuna mwabudiwa isipokuwa Allaah”. Tafsiri hii si sahihi kama ilivyo, kwa sababu kuna vitu vingi vyenye kuabudiwa badala ya Allaah (´Azza wa Jall).

Watu hawa wanakuwa wajinga zaidi kuliko wale wajinga ambao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitumwa kwao. Kwani wao walikuwa wanatambua maana ya matamshi hayo tofauti na watu hawa.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Fitqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 42
  • Imechapishwa: 23/04/2022