18. Mke anatakiwa kumtii mume wake

Miongoni mwa haki za mume juu ya mke wake ni yeye kumtii katika yasiyokuwa kumuasi Allaah na wala asijipe udhuru kwa kitu kingine chenye kubughudhi. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa kuhusu wanawake walio bora. Akasema:

“Ni yule anayemtii mume wake anapomuamrisha.”[1]

Mwanamke mwema alobarikiwa anamtii mume wake wakati anapomuamrisha kwa kutarajia kupata ushuhuda huu wa hali ya juu na uliomtukufu kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Anataka kuingia Pepo ya Mola Wake. Ambayo Amewaahidi waja Wake wema kitu ambacho hakijaonwa na jicho, hakijasikiwa na sikio na hakijafikiriwa kamwe na moyo. Anajua kuwa Mola Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwanamke akiswali Swalah zake tano, akafunga mwezi wake, akahifadhi tupu yake na akamtii mume wake, ataambiwa: “Ingia kupitia mlango wowote wa Pepo unaoutaka.”[2]

Anaogopa khasira na adhabu ya Mola Wake ikiwa atamuasi Mola Wake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu wataokuwa na adhabu kali siku ya Qiyaamaaha ni watu sampuli mbili; mwanamke aliyemuasi mume wake na kiongozi aliyewaongoza watu ambao wanamchukia.”[3]

Mwanamke wa Kiislamu anamtii mume wake kwa furaha na anaogopa kumuasi. Kwa sababu anataraji thawabu za Allaah na anaogopa adhabu Zake. Lakini pamoja na yeye kumtii mume wake anafanya hivo tu kwa yale yasiyokuwa madhambi. Ikiwa atamuamrisha kumuasi Allaah asimtii. Ikiwa atamuamrisha kustarehe naye kwa njia ya haramu asimkubalie. Ikiwa atamuamrisha kujipamba kwa njia ya haramu, kama Nams[4], asimtii. Baadhi ya wanawake wanapiga simu na kuuliza juu ya waume wanaotaka wanyoe nyusi, kurefusha nywele na kuvaa baruka [peruk]. Je, wawatii? Kwa vile haki za mume ni kubwa. Hebu tusikilize kisa hichi ili tujue kuwa haifai kwa mwanamke kumtii mume katika dhambi. Kuna mwanamke alikuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumueleza ya kwamba msichana wake ameolewa na kwamba nywele zake ni ngumu. Akasema:

“Mume wake ameniamrisha kurefusha nywele zake.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Wanawake wenye kurefusha nywele zao wamelaaniwa.”[5]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna utiifu kwa kiumbe katika kumuasi Muumba.”[6]

[1] an-Nasaaiy (3231), Ahmad (2/251) na al-Haakim (2/2682) ambaye ameisahihisha kwa mujibu wa masharti ya Muslim. Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”as-Swahiyhah” (1838) na ”al-Irwaa’” (1786).

[2] Ahmad (1661) na at-Twabaraaniy katika ”al-Awsat” (8805) ambaye amesema: ”Hadiyth hii haikupokelewa kwa njia ya mnyororo huu kutoka kwa mwengine zaidi ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf. Ibn Lahiy´ah yeye peke yake ndio ameipokea.” Ina upokezi unaoitolea ushahidi kwa Ibn Hibbaan katika ”as-Swahiyh” (4163) kupitia kwa Abu Hurayrah. al-Albaaniy ameifanyia Ta´liyq na amesema: ”Ni nzuri kupitia zingine.” Tazama ”Aadaab-uz-Zafaaf” (282) na ”at-Ta´liyq ar-Raghiyb” (3/73).

[3] at-Tirmidhiy (359) na Ibn Abiy Shaybah (1/407) kupitia ´Amr bin al-Haarith bin al-Mustwaliq (Radhiya Allaahu ´anh). Muundo ni wa at-Tirmidhiy na mnyororo wake ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika Ta´liyq yake ya at-Tirmidhiy.

[4] Nams ina maana ya kutoa nywele usoni na nyusi. Tazama ”Lisaan-ul-´Arab” na ”al-Qaamuus”.

[5] al-Bukhaariy (5202) na Muslim (2123).

[6] Ahmad (4/426), al-Haakim (3/8570) na at-Twabaraaniy (18/381) na muundo ni wake. Mnyororo ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Haakim na adh-Dhahabiy ameafikiana naye. Tazama ”as-Swahiyhah” (179) ya al-Albaaniy.

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliym ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haqq-uz-Zawjayn, uk. 29-31
  • Imechapishwa: 24/03/2017