Allaah amemtuma Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kulingania katika Tawhiyd na kukataza shirki. Akafikisha (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) yale Allaah aliyomtuma kwa njia nzuri kabisa. Aliudhiwa kwa ajili ya Allaah kwa maudhi makubwa. Pamoja na hivyo akayavumilia yeye pamoja na Maswahabah wake (Radhiya Allaahu ´anhum) katika kufikisha dini ya Allaah mpaka Allaah akaondosha katika kisiwa cha kiarabu masanamu na mizimu yote na watu wakaingia katika dini ya Allaah makundi kwa makundi. Wakayavunja masanamu yaliyokuwa pembezoni na ndani ya Ka´bah na al-Laat, al-´Uzzaa, Manaat na masanamu mengine yote yaliyokuwa katika makabila ya waarabu yakaangamizwa na kuvunjwa. Vilevile ikaangamizwa mizimu waliokuwa nayo. Neno la Allaah likanyanyuliwa na Uislamu ukadhihiri katika kisiwa cha kiarabu. Hapo sasa ndipo waislamu wakaelekea kulingania katika dini ya Allaah na kupigana Jihaad nje ya kisiwa cha kiarabu na Allaah akawaongoza kupitia wao wale waja waliotanguliwa na furaha na vilevile Allaah akaeneza haki na uadilifu kupitia wao katika sehemu kubwa ya ulimwengu. Kwa hayo wakawa ni maimamu wa uongofu na viongozi wa haki na walinganizi wa uadilifu na kutengeneza. Taabi´uun na waliowafuata kwa wema wakapita juu ya mfumo wao. Wakawa ni maimamu wa uongofu na walinganizi wa haki wenye kueneza dini ya Allaah. Wanawalingania watu katika kumuabudu Allaah peke yake na wanapambana katika njia ya Allaah. Wanafanya hivo kwa nafsi na mali zao. Hawajali kwa ajili ya Allaah lawama za wenye kulaumu. Basi Allaah akawapa nguvu, akawanusuru, akawapa ushindi juu ya wengine na akawatimizia yale Allaah aliyowaahidi katika maneno Yake (Subhaanah):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَنصُرُوا اللَّـهَ يَنصُرْكُمْ وَيُثَبِّتْ أَقْدَامَكُمْ

“Enyi mloamini! Mkimnusuru Allaah Naye atakunusuruni na ataithibitisha miguu yenu.” (47:07)

وَلَيَنصُرَنَّ اللَّـهُ مَن يَنصُرُهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ الَّذِينَ إِن مَّكَّنَّاهُمْ فِي الْأَرْضِ أَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ وَأَمَرُوا بِالْمَعْرُوفِ وَنَهَوْا عَنِ الْمُنكَرِ ۗ وَلِلَّـهِ عَاقِبَةُ الْأُمُورِ

“Bila shaka Allaah atamnusuru yule mwenye kumnusuru. Hakika Allaah ni Mwenye nguvu kabisa, Mwenye enzi. Ambao Tukiwamakinisha katika ardhi, husimamisha swalah na hutoa zakaah na huamrisha mema na hukataza maovu. Kwa Allaah pekee ndio hatima ya mambo yote.” (22:40-41)

Baada ya hapo watu wakabadilika, wakafarikiana, wakachukulia usahali suala la Jihaad, wakaipa kipaumbele raha, wakafuata matamanio na kukadhihiri kwao maovu. Waliosalimika ni wale tu waliokingwa na Allaah (Subhaanah). Allaah akawabadilikia na akawatawalishia maadui wao. Hayo ni malipo ya yale waliyoyachuma. Hakika Mola Wako si mwenye kumdhulumu mja. Amesema (Ta´ala):

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ لَمْ يَكُ مُغَيِّرًا نِّعْمَةً أَنْعَمَهَا عَلَىٰ قَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ

“Hayo ni kwa kuwa Allaah hakuwa Mwenye kubadilisha neema yoyote Aliyoineemesha kwa watu mpaka wao wabadilishe yaliyomo ndani ya nafsi zao.” (08:53)

Ni wajibu kwa waislamu wote – watawala na raia – warejee kwa Allaah (Subhaanah), wamtakasie ´ibaadah Yeye pekee, watubie Kwake kwa yale yaliyopita katika mapungufu na madhambi yao. Vilevile wanatakiwa wakimbilie zile faradhi Allaah alizowawajibishia na wajiepushe na yale aliyowaharamishia. Wausiane na wasaidiane hayo.

Katika yaliyo muhimu kuliko hayo ni kusimamisha adhabu za Kishari´ah, kuwahukumu watu kwa Shari´ah katika kila kitu na kuhukumiwa kwayo. Sambamba na hilo kanuni zilizotungwa ambazo zinapingana na Shari´ah ya Allaah zinatakiwa kutokomezwa na watu wasihukumiane nazo. Badala yake inatakiwa kuwalazimisha wananchi wote hukumu ya Shari´ah.

Ni wajibu kwa wanachuoni kuwafundisha watu dini yao, kueneza mawaidha ya Kiislamu kati yao, kuusiana katika haki na kuwa na subira juu yake. Vilevile inatakiwa kuamrishana mema na kukatazana maovu na kuwashaji´isha viongozi katika hayo.

Ni wajibu kupiga vita ujamaa, Ba´thiyyah, kuwa na kasumba juu ya mataifa na misingi mingine yenye kuangamiza na madhehebu yanayopingana na Shari´ah. Kwa hayo Allaah atawatengenezea waislamu yale yaliyoharibika na kuwazuilia yale yenye maovu na vilevile atawarudishia utukufu wao uliotangulia na kuwanusuru dhidi ya maadui wao na atawamakinisha katika ardhi. Amesema (Ta´ala):

وَكَانَ حَقًّا عَلَيْنَا نَصْرُ الْمُؤْمِنِينَ

“Ni haki daima Kwetu kuwanusuru waumini.” (30:47)

وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَىٰ لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُم مِّن بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا ۚ يَعْبُدُونَنِي لَا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئًا ۚ وَمَن كَفَرَ بَعْدَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ

“Allaah amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema kwamba: Atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyowafanya makhalifa wale waliokuwa kabla yao, atawamakinishia dini yao aliyowaridhia, atawabadilishia amani badala ya khofu yao [kwa sharti] wananiabudu Mimi pekee wasinishirikishi na chochote. Na yeyote yule atakayekufuru baada ya hapo, basi hao ndio mafasiki.” (24:55)

إِنَّا لَنَنصُرُ رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ يَقُومُ الْأَشْهَادُ

“Hakika Sisi tutawanusuru Mitume Wetu na wale walioamini katika uhai wa dunia na siku watakayosimama mashahidi.” (40:51)

يَوْمَ لَا يَنفَعُ الظَّالِمِينَ مَعْذِرَتُهُمْ ۖ وَلَهُمُ اللَّعْنَةُ وَلَهُمْ سُوءُ الدَّارِ

“Siku hazitowafaa madhalimu udhuru wao na watapata laana na watapata makazi mabaya.” (40:52)

Allaah (Subhaanah) ndiye mwenye jukumu la kuwatengeneza viongozi wa waislamu na manaibu wao, kuwatunuku uelewa katika dini, kuukusanya umoja wao juu ya uchaji Allaah, kuwahidi wote katika njia Yake iliyonyooka, kuinusuru haki kupitia wao, kuikosesha batili nusura kupitia wao, awaongoze wote kuweza kushirikiana katika wema na uchaji Allaah, kuusiana katika haki na kuwa na subira juu yake. Hakika Yeye ndiye muweza wa hayo.

Swalah na amani zimwendee mja, Mtume Wake na kiumbe bora, Mtume wetu, kiongozi wetu na bwana wetu Muhammad bin ´Abdillaah, kizazi chake, Maswahabah wake na wenye kufuata uongofu wake.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah as-Swahiyhah wa maa yudhwaadduhaa, uk. 17
  • Imechapishwa: 31/05/2023