18. Allaah amewaumba viumbe kwa malengo na hawakuachwa burebure

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

La kwanza: Allaah Ametuumba, akaturuzuku na Hakutuacha bure tu bila ya malengo.

MAELEZO

La kwanza – Ametuumba baada ya kuwa hatupo. Hatukuwa chochote kabla Yeye kutuumba. Amesema (Ta´ala):

هَلْ أَتَىٰ عَلَى الْإِنسَانِ حِينٌ مِّنَ الدَّهْرِ لَمْ يَكُن شَيْئًا مَّذْكُورًا

”Je, mtu hakufikiwa na kipindi fulani katika dahari, hakuwa kitu kinachotajwa?”[1]

قَالَ كَذَٰلِكَ قَالَ رَبُّكَ هُوَ عَلَيَّ هَيِّنٌ وَقَدْ خَلَقْتُكَ مِن قَبْلُ وَلَمْ تَكُ شَيْئًا

“Akasema: “Namna hiyo Mola wako amesema: “Haya ni sahali Kwangu na kwani nilikwishakukuumba kabla na wala hukuwa chochote.”[2]

Mtu hakuwa chochote kabla ya kuumbwa. Ambaye amemuumba ni Allaah (´Azza wa Jall). Amesema (Ta´ala):

أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ

“Au wameumbwa pasi po na kitu chochote au wao ndio waumbaji.”[3]

Akaturuzuku – Pale tulipokuwa ni wenye kuhitajia riziki kama chakula, kinywaji, mavazi, makazi, vipando na manufaa Allaah (Subhaanah) akajua haja zetu na hivyo akatufanyia wepesi vilivyomo mbinguni na ardhini. Vyote hivo viko kwa ajili ya manufaa yetu ili tuweze na ili viweze kutusaidia kwa kile ambacho Allaah ametuumba kwa ajili yake. Nacho si kingine ni kumwabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Hakutuacha bure – Kuachwa bure ni kitu kilichopuuzwa kisichopewa umuhimu. Allaah ametuumba na akaturuzuku kwa ajili ya hekima. Hakutuumba kimchezomchezo wala burebure. Amesema (Ta´ala):

أَفَحَسِبْتُمْ أَنَّمَا خَلَقْنَاكُمْ عَبَثًا وَأَنَّكُمْ إِلَيْنَا لَا تُرْجَعُونَ

“Je, mlidhania kwamba Sisi Tulikuumbeni bila kusudio mcheze tu na kwamba nyinyi Kwetu hamtorejeshwa?”[4]

أَيَحْسَبُ الْإِنسَانُ أَن يُتْرَكَ سُدًى أَلَمْ يَكُ نُطْفَةً مِّن مَّنِيٍّ يُمْنَىٰ ثُمَّ كَانَ عَلَقَةً فَخَلَقَ فَسَوَّىٰ

”Je, anadhani insani ataachwa huru bila jukumu? Kwani hakuwa tone kutokana na manii yanayomwagwa kwa nguvu? Kisha akawa pande la damu, (Allaah) Akamuumba na Akamsawazisha?”[5]

وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاءَ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا بَاطِلًا ۚ ذَٰلِكَ ظَنُّ الَّذِينَ كَفَرُوا ۚ فَوَيْلٌ لِّلَّذِينَ كَفَرُوا مِنَ النَّارِ

“Hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake pasipo malengo – hiyo ndio dhana ya wale waliokufuru; basi ole wale waliokufuru kwa moto utakaowapata.”[6]

Allaah ametuumba na akatuumbia riziki hizi na nyenzo kwa ajili ya hekima na lengo kubwa ambalo ni kumwabudu Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala). Hakutuumba kama wanyama ambao wameumbwa kwa ajili ya manufaa ya waja kisha wanakufa na kupotea. Kwa sababu hakufaradhishiwa ´ibaadah yoyote, hakuamrishwa wala kukatazwa kitu. Ametuumba ili tumwabudu. Amesema (Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ مَا أُرِيدُ مِنْهُم مِّن رِّزْقٍ وَمَا أُرِيدُ أَن يُطْعِمُونِ إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الرَّزَّاقُ ذُو الْقُوَّةِ الْمَتِينُ

“Sikuumba majini na wana Aadam isipokuwa waniabudu. Sitaki kutoka kwao riziki yoyote na wala Sitaki wanilishe. Hakika Allaah ndiye Mwingi wa kuruzuku, Mwenye nguvu madhubuti.”[7]

Hakutuumba kwa ajili tu ya kuishi katika maisha haya ya dunia ambapo tuishi, tule raha, tule, tunywe na tujitanafasi na eti baada yake hakuna kitu. Maisha haya ni shamba na soko kwa ajili ya nyumba ya Aakhirah. Ndani yake tunachuma akiba ya matendo mema kisha tunakufa na kutoka ndani yake, kisha tunafufuliwa, kisha tunafanyiwa hesabu na kulipwa kwa matendo yetu. Hili ndio lengo la kuumbwa kwa watu na majini. Dalili ya hayo ni Aayah nyingi zinazofahamisha juu ya kufufuliwa, kukusanywa, kulipwa na kufanyiwa hesabu. Akili pia inafahamisha hivo. Hailingani na hekima ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kuumba uumbaji huu wa kushangaza na kuwawepesishia ulimwengu huu wanaadamu kisha akawaacha wakafa na kupotea bila natija yoyote. Huu ni mchezo. Ni lazima matokeo ya matendo haya yadhihirike katika nyumba ya Aakhirah. Kwa ajili hiyo wapo watu ambao wanayatumia maisha yao yote katika kumwabudu na kumtii Allaah na wakati huohuo ni fukara na muhitaji na anaweza kuwa ni mwenye kudhulumiwa na akinyanyaswa na asipate kitu katika malipo ya matendo yake hapa duniani. Upande mwingine watu wengine wakawa ni makafiri, wakanamungu na waovu ambao wanastarehe na kujifurahisha katika maisha haya ya dunia, anapata kile anachokitaka, anafanya yale aliyoharamisha Allaah, anawadhulumu waja, anawashambulia, kula mali zao, anawaua pasi na haki, anawasaliti na kuwafanyia jeuri kisha akafa katika hali hiyo bila ya kufikwa na kitu katika adhabu. Je, hivi kweli inalingana kwa uadilifu na hekima ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kumwacha kafiri huyu bila ya kumlipa? Hili haliendani na uadilifu Wake (Subhaanahu wa Ta´ala). Kwa ajili hiyo ndio maana akatenga nyumba nyingine ambapo atamlipa mtenda mema kwa wema wake na mtenda maovu kwa uovu wake. Huko ndio kutadhihiri matunda ya matendo. Dunia ni nyumba ya matendo. Kuhusu Aakhirah ni nyumba ya malipo; ima Pepo au Moto. Hakutuacha hivi burebure kama wanavyofikiria makafiri na wenye kuamini mazingira. Amesema (Ta´ala):

وَقَالُوا مَا هِيَ إِلَّا حَيَاتُنَا الدُّنْيَا نَمُوتُ وَنَحْيَا وَمَا يُهْلِكُنَا إِلَّا الدَّهْرُ ۚ وَمَا لَهُم بِذَٰلِكَ مِنْ عِلْمٍ ۖ إِنْ هُمْ إِلَّا يَظُنُّونَ

“Wakasema: “Huu si chochote isipokuwa ni uhai wetu wa dunia, tunakufa na tunahuika na hakuna kitachotuangamiza isipokuwa zama tu; na wala hawana kwayo ujuzi wowote, si vyenginevyo isipokuwa wao wanadhania tu.”[8]

Haya ni maneno ya wakanamungu ambao hawaamini kufufuliwa na kukusanywa.

Allaah (´Azza wa Jall) amewakemea na kusema:

أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ اجْتَرَحُوا السَّيِّئَاتِ أَن نَّجْعَلَهُمْ كَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ سَوَاءً مَّحْيَاهُمْ وَمَمَاتُهُمْ ۚ سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ

“Je, wanadhania wale waliochuma mabaya Tuwafanye wawe sawa na wale walioamini na wakatenda mema na pia sawasawa uhai wao na kufa kwao? – uovu ulioje wanaouhukumu!”[9]

أَمْ نَجْعَلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ كَالْمُفْسِدِينَ فِي الْأَرْضِ أَمْ نَجْعَلُ الْمُتَّقِينَ كَالْفُجَّارِ

“Je, Tuwajaalie wale walioamini na wakatenda mema kama wenye kueneza ufisadi ardhini au tuwajaalie wachaji kama waovu?”[10]

[1] 76:01

[2] 19:09

[3] 52:35

[4] 23:115

[5] 75:36-38

[6] 38:27

[7] 51:56-58

[8] 45:24

[9] 45:21-22

[10] 38:28

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 43-45
  • Imechapishwa: 01/12/2020