Wakati maiti anapolazwa ndani ya kaburi lake akafukiwa na watu wakaondoka zao, husikia nyayo za viatu vyao, kama inavosema Hadiyth. Roho yake hurudishwa katika kiwiliwili chake. Haya ni maisha ya ndani ya kaburi ambayo hakuna ayajuaye isipokuwa Allaah. Allaah juu ya kila jambo ni muweza. Baada ya roho yake kurudishwa katika kiwiliwili chake na akapewa uhai mwingine, hujiliwa na Malaika wanaomuhoji maswali matatu: Ni nani Mola wako? Ni ipi dini yako? Ni nani Mtume wako?[1] Akijibu majibu sahihi, basi hufuzu na akashinda ambapo kaburi lake likawa ni bustani miongoni mwa mabustani ya Peponi kisha siku ya Qiyaamah akawa miongoni mwa watu wa Peponi. Na akishindwa kujibu, basi kaburi lake linakuwa ni shimo miongoni mwa mashimo ya Motoni. Kaburi lake hufanywa kumbana mpaka zikakutana mbavu zake[2]. Yule wa mwanzo hupanuliwa kaburi lake kiasi cha macho yanapofika na akafunguliwa mlango miongoni mwa milango ya Peponi ambapo akajiliwa na rehema na harufu yake nzuri. Huyu mwingine kaburi lake humbana mpaka zikakutana mbavu zake na akafunguliwa na mlango wa Motoni ambapo akajiliwa na joto na sumu zake.

Jibu sahihi ambalo Allaah humthibitisha mwenye nalo ni yeye kusema: Mola wangu ni Allaah, dini yangu ni Uislamu na Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye Mtume wangu:

يُثَبِّتُ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ

“Allaah huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika maisha ya duniani na Aakhirah.”[3]

Jawabu sahihi ni kwa sababu ya kumwamini kwake Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), na si kwa sababu ya kujifunza na utamaduni. Asiyekuwa na imani hatoweza kujibu sahihi. Mnafiki, ambaye alidhihirisha imani na akaficha ukafiri dunaini, ndiye ambaye hatoweza kujibu sahihi. Badala yake atasema:

“Eeh, eeh. Sijui. Niliwasikia watu wakisema kitu nami nikakisema.” Hapo ndipo atapigwa nyundo ya chuma, lau nyundo hiyo ingepigwa kwenye mlima basi ungesambuka. Atapiga ukelele mkubwa ambao anasikiwa na kila kiumbe cha Alllaah isipokuwa watu na majini. Endapo watu na majini wangelimsikia basi wangelikufa.”[4]

وَيُضِلُّ اللَّـهُ الظَّالِمِينَ ۚ وَيَفْعَلُ اللَّـهُ مَا يَشَاءُ

“… na Allaah huwaacha kupotoka madhalimu; na Allaah anafanya akitakacho.”[5]

[1]Ahmad (4/287) na (4/295), Abu Daawuud (4753) na al-Haakim (1/37-40) ambaye ameisahihisha.

[2]Ahmad (4/287) na Abu Daawuud (4753).

[3]14:27

[4]Ahmad (4/287) na Abu Daawuud (4753).

[5]14:27

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 194-195
  • Imechapishwa: 10/12/2024