2 na 3- Kujipiga mashavu na kupasua nguo. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Si katika sisi yule mwenye kujipiga kwenye mashavu, kupasua nguo na akatamka matamshi ya kipindi cha kishirikina.”

Ameipokea al-Bukhaariy (03/127-128,129), Muslim (01/70), Ibn Jaaruud (257), al-Bayhaqiy (04/63-64) na wengineo kupitia kwa Ibn Mas´uud.

4- Kunyoa nywele. Abu Burdah bin Abiy Muusa ameeleza:

“Abu Muusa alipatwa na maumivu makali ambapo akazimia na kichwa chake kilikuwa kwenye mapaja ya mmoja wa wake zake. Mmoja katika wake zake akapiga makelele na hakuweza kumjibu chochote. Wakati alipozindukana akasema: “Hakika mimi najitenga mbali na yule ambaye Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alijitenga naye mbali. Hakika Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amejitenga mbali na mwanamke mwenye kuinua sauti, mwanamke mwenye kunyoa nywele zake na mwanamke mwenye kupasua nguo zake wakati wa msiba.”

Ameipokea al-Bukhaariy (03/129), Muslim (01/70), an-Nasaa´iy (01/263) na al-Bayhaqiy (04/64).

5- Kuzifanya nywele kuwa timtim. Hayo ni kutokana na Hadiyth moja miongoni mwa wale wanawake waliokula kiapo cha usikivu kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesimulia:

“Miongoni mwa ahadi alizochukua kwetu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika mambo mema ambayo alichukua kwetu: ni kwamba tusimwasi juu yake, tusirarue nyuso zetu kwa kucha, tusijiombee maangamivu, tusipasue nguo na wala tusizifanye nywele kuwa hovyohovyo.”

Ameipokea Abu Daawuud (02/59) na al-Bayhaqiy kupitia njia zake kwa cheni ya wapokezi nzuri.

6- Baadhi ya wanaume kufuga nywele zao masiku machache kwa sababu ya kuonyesha huzuni juu ya maiti wao. Yanapomaisha masiku hayo anarudi kuzinyoa. Ufugaji wa sampuli hii[1] unaingia ndani ya maana ya kuzifanya nywele kuwa timtimt, kama ilivyo dhahiri. Aidha kitendo hicho ni Bid´ah. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kila Bid´ah ni upotevu na kila upotevu ni Motoni.”

Ameipokea an-Nasaa´iy na al-Bayhaqiy katika “al-Asmaa´ was-Swiffaat” kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kupitia kwa Jaabir, kama ilivyotangulia katika kurasa ya 18.

7- Kutangaza juu ya kifo cha maiti wake kupitia minara na mfano wake. Kwa sababu kitebdo hicho ni katika Na´y. Imethibiti kwa Hudhayfah bin al-Yamaan (Radhiya Allaahu ´anh) kwamba amesema:

“Alikuwa anapofiwa an maiti husema: “Msimjulishe yeyote. Hakika mimi nachelea isije ikawa ni Na´y. Hakika mimi nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akikataza watu Na´y.

Ameipokea at-Tirmidhiy (02/129) na ameifanya kuwa nzuri, Ibn Maajah (01/450), Ahmad (05/406) na mtiririko ni wake, al-Bayhaqiy (04/74). Vilevile Ibn Abiy Shaybah ameipokea kwa kuirufaisha kutoka kwake katika “al-Muswannaf” (04/98). Cheni ya wapokezi wake ni nzuri, kama alivosema al-Haafidhw katika “al-Fath”.

Na´y maana yake kilugha ni kutoa khabari kuhusu kifo cha maiti. Kutokana na haya kunaingia khabari zote. Lakini kumepokelewa Hadiyth Swahiyh zinazoonyesha kuwa aina fulani ya utoaji wa khabari inafaa. Kwazo wanachuoni wamefungamanisha makatazo na wamesema kuwa makusudio ya Na´y (iliyokatazwa) ni utoaji wa khabari ambao unafanana na yale yaliyokuwa yakifanywa katika kipindi kabla ya kuja Uislamu katika kupiga mayowe kwenye milango ya majumba na masoko, kama itavyokuja huko mbele. Kwa ajili hiyo nasema:

[1] Msingi wa kufuta ndevu ni kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama ilivyo wazi. Ni Sunnah ambayo ni ya wajibu ambayo wengi wa watu wameizembea. Tazama ”Aadad-uz-Ziffaaf, uk. 208-213.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 42-44
  • Imechapishwa: 07/01/2020