مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِنْدَهُ إِلاَّ بِإِذْنِهِ

“Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake?” (02:255)

Bi maana hakuna yeyote atayeombea mbele Yake siku ya Qiyaamah isipokuwa kwa idhini Yake. Mitume na waja wema wataombea baada ya kupata idhini Yake (Subhaanahu wa Ta´ala).

Kuhusiana na duniani Allaah (Subhaanah) amewaamrisha watu wote wamuombe Yeye pekee du´aa na wawaombee uombezi ndugu zao duniani kwa ajili ya Allaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anaombea pindi anapotakwa uombezi. Pindi mmoja katika watu anapomuomba uombezi na amtatulie tatizo anamuombea (´alayhis-Swalaatu was-Salaam)[1].

Lakini siku ya Qiyaamah hakuna yeyote atayeombea uombezi isipokuwa kwa idhini Yake (Subhaanahu wa Ta´ala). Ama duniani wanaombea kwa idhini Yake ya kijumla. Kwa sababu ameidhinisha katika Shari´ah waumini kuombeana idhini kati yao. Amesema (Ta´ala):

مَّن يَشْفَعْ شَفَاعَةً حَسَنَةً يَكُن لَّهُ نَصِيبٌ مِّنْهَا ۖ وَمَن يَشْفَعْ شَفَاعَةً سَيِّئَةً يَكُن لَّهُ كِفْلٌ مِّنْهَا

“Atakayeombea uombezi mzuri atapata fungu lake, na atakayeombea uombezi mbaya atapata sehemu yake.” (04:85)

Amewaidhinisha (Subhaanah) na kuwasisitiza kufanya hivo; wasaidiane katika wema na uchaji Allaah, wapeana nasaha na kuusiana kwa haki. Uombezi unaingia katika kuusiana kwa haki na ni katika kufanya wema. Uombezi unajuzu duniani kwa idhini Yake (Subhaanah) ya kijumla. Ama kuhusu Aakhirah uombezi hautofaa isipokuwa baada ya kupata idhini Yake maalum. Hakuna yeyote atayeombea isipokuwa kwa idhini Yake (Subhaanah). Kwa ajili hii watu siku ya Qiyaamah watamwendea Aadam, Nuuh, Ibraahiym, Muusa na ´Iysaa (´alayhimus-Salaam) ambapo wote wataomba udhuru. Hatimaye waende kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) asujudu mbele ya Mola Wako chini ya ´Arshi, kisha amhimidi Allaah kwa himdi kubwa na halafu baada ya hapo ndio ampe idhini na kumwambia:

“Ombea utakubaliwa maombi yako.”

[1] Tazama al-Bukhaariy (5652) na Muslim (2576).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 24-25
  • Imechapishwa: 19/10/2024