Ahmad (Rahimahu Allaah), Abu Daawuud (Rahimahu Allaah) na an-Nasaa’iy (Rahimahu Allaah) wamepokea kupitia kwa Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh), ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah haachi kumgeukia mja wakati wa kuswali kwake muda wa kuwa hajageuka. Akigeuka humwondokea.”[1]

Imaam Ahmad na at-Tirmidhiy wamepokea kupitia kwa al-Haarith al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anh), ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah alimwamrisha Yahyaa bin Zakariyyaa mambo matano… Nakuamrisheni swalah. Allaah huweka uso Wake mbele ya uso wa mja Wake muda wa kuwa hajageuka.”[2]

Zipo Hadiyth zingine nyingi zenye maana kama hiyo.

`Atwaa’ amesimulia kuwa alimsikia Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anh) akisema:

“Anaposwali mmoja wenu basi asigeuke, kwani anamnong´oneza Mola wake. Mola wake yuko mbele yake na yeye anamnong´oneza. Hivyo basi asigeuke.”

`Atwaa’ (Rahimahu Allaah) amesema:

“Tumefikiwa na khabari kwamba Mola (‘Azza wa Jall) anasema: “Ee Mwanadamu! Unamgeukia kwa faida gani? Mimi ni bora kwako kuliko yule unayemgeukia.”

al-Bazzaar na wengine wamepokea kwa njia ya masimulizi ya kinabii. Hata hivyo Swahiyh zaidi ni kwamba ni masimulizi ya Swahabah.

Abu ´Imraan al-Juuniy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Allaah (‘Azza wa Jall) alimteremshia wahy Muusa (‘alayhis-Salaam): “Ee Muusa! Unaposimama mbele Yangu, basi simama kama mja masikini na mtwevu. Jilaumu nafsi yako, kwa sababu ina haki zaidi ya kulaumiwa. Ninong´oneze kwa moyo wenye aibu na ulimi wa kweli.”[3]

[1] Ahmad (5/172), Abu Daawuud (909) na an-Nasaa’iy (1195). Swahiyh kwa mujibu wa Ibn Khuzaymah (1/244) na al-Haakim (1/361). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan Abiy Daawuud” (909).

[2] Ahmad (5/849-850) na at-Tirmidhiy (2863), ambaye amesema kuwa Hadiyth ni nzuri, Swahiyh na ngeni. Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy” (2863).

[3] Hilyat-ul-Awliyaa’ (5/66).

  • Muhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn ´Abdur-Rahmaan bin Rajab al-Hanbaliy (afk. 795)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Khushuu´ fiys-Swalaah, uk. 72-74
  • Imechapishwa: 24/11/2025