17. Kasoro ya Hadiyth (علل الحديث) – moja ya elimu tukufu

Makusudio kama tulivyosema ni kwamba Hadiyth iliyosimuliwa kwa njia nyingi, bila ya kuwa mpango  wa kukubaliana au maelewano hapo kabla, kikawaida inapelekea elimu ya kile kilichonakiliwa. Isitoshe jambo hili ni lenye manufaa sana inapokuja katika hali za wasimulizi. Katika hali hii kuna faida katika masimulizi yaliyopokelewa na watu wasiotambulika, watu wenye kumbukumbu dhaifu, cheni zisizokuwa na Swahabah na mfao wake. Kwa sababu hii wanazuoni walikuwa wakiandika Hadiyth kama hizo na kusema kwamba zinafaa katika hali na lengo la kutilia nguvu na mazingatio na si katika hali na malengo mengine. Ahmad amesema kuwa wakati mwingine alikuwa anaweza kuandika Hadiyth ya mtu kwa ajili ya kuizingatia[1]. Akatolea mfano wa hakimu wa Misri ´Abdullaah bin Lahiy´ah. Alikuwa ni miongoni mwa wapokezi waliokuwa na Hadiythi nyingi na alikuwa ni miongoni mwa watu bora kabisa. Hata hivyo baada ya vitabu vyake kuungua, baadhi ya Hadiyth zake za baadaye zilipatikana na makosa. Kwa hivyo akawa anamtumia kama mazingatio na kusimulia kutoka kwake kwa lengo la kutilia nguvu. Mara nyingi alikuwa akimuambatanisha na al-Layth bin Sa’d, ambaye alikuwa thabiti na imamu mwenye hoja madhubuti.

Vilevile kama jinsi wanavyotumia Hadiyth za wapokezi wenye kumbukumbu dhaifu kwa lengo la kutilia nguvu na mazingatio, walikuwa pia wanaweza kuzidhoofisha Hadiyth za wapokezi waaminifu, wakweli na madhubuti, pale ambapo, kwa kutumia msaada wa mambo mbalimbali,wanagundua kuwa walikosea katika kusimulia. Waliita elimu hiyo kuwa ni elimu ya kasoro ya Hadiyth (علل الحديث) na ilikuwa ni miongoni mwa elimu zao tukufu. Kwa namna ya kwamba Hadiyth inaweza kuwa imesimuliwa na msimulizi mwaminifu na madhubuti, lakini bado amekosea. Kosa lake linaweza kutambulika kwa sababu zilizo wazi. Kwa mfano ni kama walivyojua kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuoa Maymuunah wakati alipokuwa ameshatoka ndani ya Ihraam[2] na kwamba aliswali Rak´ah mbili kwenye Nyumba. Kwa namna hiyo waliweza kuthibitisha upokezi wa Ibn ´Abbaas unaosema kuwa alimuoa akiwa ndani ya Ihraam[3] na kwamba hakuswali ni wa makosa. Kwa vile yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifanya ´Umrah nne hivyo wakatambua kuwa upokezi wa Ibn ´Umar unaosema kuwa alifanya ´Umrah katika Rajab[4] ni wa makosa. Kwa vile alifanya hijjah ya Tamattu´, wakati wa Hijjah ya Kuaga, wakiwa ndani ya amani na hivyo wakatambua kuwa maneno ya ´Uthmaan alipomwambia ´Aliy ”Tulikuwa kipindi hicho ni wenye khofu”[5] kuwa alikosea. Kadhalika katika upokezi mmoja wa al-Bukhaariy, unaosema kwamba Moto hautojaa mpaka pale Allaah atapouumbia viumbe wapya[6], ni wa makosa. Ipo mifano mingi kama hiyo.

[1] Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (8/16).

[2] at-Tirmidhiy (841).

[3] al-Bukhaariy (4258-4259) na Muslim (1410).

[4] al-Bukhaariy (1775-1776).

[5] al-Bukhaariy (1563-1569).

[6] al-Bukhaariy (4849-4850) na Muslim (2846).

  • Muhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Muqaddimah fiy Usuwl-it-Tafsiyr, uk. 62-66
  • Imechapishwa: 02/04/2025